March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MWAUWASA yasaini mkataba wa kuboresha mfumo wa majitaka,kulinda Ziwa Victoria

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) imesaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa kuboresha mfumo rahisi wa uondoshaji majitaka maeneo ya milimani jijini Mwanza ili kuimarisha usafi wa mazingira na kulinda Ziwa Victoria.

Mkataba huo wa nyongeza wenye thamani ya Euro milioni 7.86 (bilioni 22 TZS) umesainiwa kati ya MWAUWASA na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), ukishuhudiwa na viongozi wa Serikali walioongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa.

Mradi utawezesha upanuzi wa mtandao wa majitaka katika maeneo ya Kiseke, Lumala na Ilemela kwa ulazaji wa kilomita 25 za mabomba, maunganisho mapya kwa takribani kaya 1,800.

Pia taasisi na majengo ya kibiashara, ujenzi wa kituo cha kusukuma majitaka, ujenzi wa maabara maalum na ununuzi wa magari mawili ya kunyonya majitaka.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo la utiaji saini,Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA Neli Msuya,amesema mamlaka hiyo itaendelea kusimamia mradi kwa umakini, kushirikisha jamii na kuhakikisha uendelevu wa uwekezaji huo, huku akitambua mchango wa Wizara ya Maji kupitia Waziri Jumaa Aweso na Katibu Mkuu.

Neli ametumia fursa hiyo kuwashukuru wadau wa maendeleo, Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na Umoja wa Ulaya (EU), akibainisha kuwa mradi huo ni matokeo ya sera na diplomasia njema ya Serikali.

Katibu Mtendaji Jumuiya ya Afrika Mashariki LVBC, Dkt. Masinde Bwire, amesema mradi huo unaotekelezwa kwa programu ya kikanda unalenga kudhibiti uchafuzi wa Ziwa Victoria ambalo ni rasilimali muhimu kwa nchi za Jumuiya hiyo katika maji, uvuvi, nishati na uchumi wa wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa, amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi na kuwataka wananchi kulinda miundombinu na kulipia ankra( bill) za huduma kwa wakati ili huduma iwe endelevu.

Awali, mradi huo ulitekelezwa katika maeneo ya Kabuhoro, Pasiansi, Kilimahewa A & B, Mabatini, Igogo Sahara, Igogo Bugando, Kitangiri na Isamilo ya Nyakabungo.