Na Esther Macha, TimesMajira Online, Chunya
KUTOKANA na changamoto ya upatikanaji wa maji wilayani Chunya mkoani Mbeya, Halmashauri ya Wilaya hiyo imeanza kuchimba visima vya maji, huku baadhi yake tayari vimekamilika katika shule za sekondari, hatua inayolenga kukabiliana na uhaba wa maji uliokuwa ukiwakabili wanafunzi na kuathiri mazingira ya kujifunzia.
Akizungumza Januari 9, 2026, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Athumani Bamba amesema kuwa halmashauri hiyo imekuwa ikitumia kila fursa ya upatikanaji wa bajeti kuchimba visima vya maji ili kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma ya maji na kuweza kusoma kwa utulivu.
“Sasa hivi tunajitahidi kila tunapopata fedha, tunachimba visima. Tumeanza katika sekta ya elimu, hasa shule za sekondari ambako kulikuwa na changamoto kubwa. Watoto wako mabwenini lakini hawakuwa wakipata maji. Tumeanza na shule za Isenyela, Kiwanja, Chokaa na Makongolosi, na hizi zote ni fedha za ndani tunazokusanya. Lengo ni kuboresha mazingira ya elimu,” amesema Bamba
Ameongeza kuwa lengo la mpango huo ni kuboresha sekta ya elimu kwa kuhakikisha shule zote za bweni zinakuwa na visima vya maji, ili wanafunzi wasikumbane na adha ya uhaba wa maji, huku mpango huo ukitarajiwa pia kuifikia shule za msingi.
“Shule zote za serikali zenye mabweni tunatarajia ziwe na visima vya maji. Tayari katika Shule ya Sekondari Mayeka visima vimechimbwa. Aidha, tunapanga kuchimba visima katika shule zote za msingi ili nazo ziwe na uhakika wa maji. Kila mwaka, bajeti yetu itaendelea kuelekezwa katika kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kutosha kama sehemu ya mkakati wa Serikali kuboresha elimu,” amesema.
Kwa upande wake, mkazi wa wilaya ya Chunya, Mary Mwasanyila, amesema hatua ya halmashauri kuchimba visima vya maji katika shule za sekondari imeleta faraja kubwa kwa jamii na manufaa kwa wanafunzi waliokuwa wakipata changamoto ya kutafuta maji kwa umbali mrefu.
“Hapo awali watoto walikuwa wanapata shida kubwa ya maji. Mtoto badala ya kuwaza masomo, anabaki kuwaza atapataje maji, na walikuwa wakitembea umbali mrefu, hali iliyokuwa ikihatarisha usalama wao. Tunashukuru sana kwa hatua hii, tunaamini italeta mabadiliko makubwa hasa katika ufaulu wa wanafunzi,” amesema.
Naye Lucy Philimon, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Isenyela wilayani Chunya, amesema kisima cha maji kilichochimbwa kitakuwa msaada mkubwa katika kukabiliana na uhaba wa maji uliokuwepo awali.
“Zamani tulikuwa tunatumia muda mwingi kutafuta maji umbali mrefu. Uwepo wa visima hivi utatufanya tuzingatie masomo zaidi. Tunazishukuru sana jitihada za Halmashauri ya Wilaya ya Chunya katika kuhakikisha tunapata elimu bora,” amesema.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi