Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amemuagiza mkandarasi wa mradi wa kuboresha usambazaji wa maji katika Jiji la Mwanza, kampuni ya Sinohydro Corporation Ltd,kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo pamoja na kuboresha mazingira rafiki kwa wafanyakazi wake.
Ambapo mazingira rafiki ni pamoja na kuhakikisha ndani ya siku saba anawaoa wafanyakazi wote wa mradi huo mikataba mipya ya ajira itakayozingatia mshahara mpya wa kima cha chini wa shilingi 515,000 kama ulivyotangazwa na Serikali.
Kundo ametoa agizo hilo baada ya kutembelea mradi huo unaohusisha ujenzi wa matenki matano yenye uwezo wa lita milioni 31 za maji na vituo viwili vya kusukuma maji na kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyakazi hao ambao Moja ya malalamiko yao ni pamoja na kutopewa mikataba mipya ya kazi.
Mhandisi Kundo amesisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitangaza mishahara mipya baada ya kutambua adha wanazopitia Watanzania, hivyo ni lazima agizo hilo litekelezwe kikamilifu kuanzia Januari 2026 bila visingizio.
Ameelekeza pia mikataba hiyo iandikwe kwa lugha ya Kiswahili ili wafanyakazi waielewe, wapatiwe usafiri salama wa kwenda na kurudi kazini, na taratibu za kinidhamu ikiwemo kufukuza wafanyakazi zizingatie sheria, huku akisisitiza kuwa changamoto zote za wafanyakazi hao lazima zitatuliwe.
“Mkandarasi uongeza nguvu kazi, kufanya kazi usiku na mchana na kuhakikisha mnatengeneza mazingira rafiki kwa wafanyakazi wenu ikiwemo kuboresha mishahara wa kima cha chini,”amesema Mhandisi Kundo.
Pia ametoa maelekezo kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA)kupitia idara ya rasilimali watu na mwanasheria kuhakikisha mikataba ya wafanyakazi katika mradi huo inazingatia Sheria ya Kazi, ikiwemo kima cha chini cha mshahara cha shilingi 515,000 kwa mwezi.
“Hakutakuwa na chembechembe za unyonyaji. mikataba iandaliwe kwa Kiswahili na Kiingereza ili wafanyakazi wafahamu wanachosaini.Pi na nyinyi wafanyakazi timizeni wajibu wenu,” amesema Mhandisi Kundo.
Naye mmoja wa mafundi katika mradi huo eneo la kituo cha kusukuma maji Sahwa,Frank Mussa,ameleza kuwa baada ya Naibu Wazuri wa Maji,kutoa maelekezo ya kutatua changamoto zilizokuwa zinawakabili wanaimani jambo hilo litafanyiwa kazi na Serikali.
“Wajaribu tu kulifuatilia kama limefanyiwa kazi agizo hilo ,lakini hatua ya kiongozi huyo kutoa maelekezo imetutia faraja na sisi wenyewe tutachapa kazi,”amesema Mussa.
Huku John Joseph,amemuomba kiongozi huyo kuwatembelea mara kwa mara katika mradi huo ili waweze kupata kipato cha kukidhi mahitaji ya familia zao na kuongeza morali ya kufanya kazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA),Neli Msuya, amesema mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya bilioni 46 na umefikia asilimia 40 ya utekelezaji wake.
Neli amesema,usanifu wa mradi huo umezingatia jiografia ya mji wa Mwanza ili kuhudumia kwa uhakika wakazi wa maeneo ya miinuko ambayo yamekuwa yakikabiliwa na upungufu wa maji.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi