Na Esther Macha, Timesmajira Online , Mbeya
KATIKA juhudi za kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya msingi ya elimu, wazazi na walezi Jijini Mbeya wametakiwa kuwahudumia watoto wao mahitaji madogo madogo ya shule ili waweze kuwa na utulivu darasani na kuongeza ufaulu.
Wito huo umetolewa Januari 10, 2026 na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbunge wa Jimbo la Uyole na Dkt. Tulia Ackson, wakati akikabidhi vifaa vya shule kwa wanafunzi 3,000 wanaotoka katika mazingira magumu jimboni humo.
Dkt. Tulia amesema kuwa mafanikio ya mwanafunzi yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya mzazi, mwalimu na mwanafunzi mwenyewe kwa kuzingatia bidii, nidhamu na mazingira bora ya kujifunzia.

“Wazazi tushirikiane katika zoezi hili. Kupata vifaa vya shule ni jambo moja, lakini mtoto kufanya vizuri ni jambo lingine. Tunawahimiza wazazi kuhakikisha watoto wote wanakwenda shule bila kikwazo chochote, hasa kutokana na kukosa sare au daftari,” amesema Dkt. Tulia.
Ameeleza kuwa sare za shule zilizotolewa zina ubora wa hali ya juu ili kuwafanya watoto wanaotoka katika familia zisizojiweza wajione sawa na wenzao na kuondoa hisia za unyonge zinazoweza kuathiri utendaji wao darasani.
“Tunataka kila mtoto wa Jimbo la Uyole atabasamu akiwa shuleni. Pale mzazi anaposhindwa, atoe taarifa ili tushirikiane kutatua changamoto. Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na daftari na sare za shule kwa wanafunzi 3,000 kutoka mitaa 60 ya jimbo lenye kata 13,” ameongeza.
Kwa upande wake, Ofisa Mawasiliano wa Taasisi ya Tulia Trust, Joshua Mwakanolo, amesema mpango wa kuwatambua watoto wanaoishi katika mazingira magumu ulihusisha wananchi moja kwa moja ili kuhakikisha wanafunzi wanafikiwa kwa usahihi.
Ameeleza kuwa mchakato wa mwaka wa fedha 2025/2026 ulifanyika kwa mfumo tofauti na misimu iliyopita kwa lengo la kurahisisha utambuzi wa watoto kulingana na maeneo wanayoishi.
“Hii ilirahisisha Taasisi ya Tulia Trust kuwafikia wanafunzi kwa ufanisi zaidi.Zoezi la kuwatambua hadi kushona sare lilichukua miezi miwili na limekamilika kwa wakati,” amesema Mwakanolo.
Ameongeza kuwa wanafunzi wengi wanaonufaika wanatoka katika familia za wakulima wadogo na wengine wazazi wao hufanya vibarua ili kuwapatia watoto wao elimu. Ameshauri kuwepo kwa mkakati wa kusaidia familia hizo kiuchumi kupitia kilimo ili zijikwamue zaidi.
Mmoja wa wazazi walionufaika, Magret Mwafongo, mkazi wa Itezi Magharibi, amesema msaada huo ni faraja kubwa kwake kwani alikuwa anakabiliwa na changamoto ya kuwapatia watoto wake mahitaji ya shule.
Kwa upande wake, Lucy Jackson, mwanafunzi wa Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Itezi, amesema msaada huo utamsaidia kufanya vizuri zaidi masomoni na amewaomba viongozi wengine kuiga mfano wa Dkt. Tulia kwa kusaidia watoto wanaotoka katika familia zisizojiweza.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi