*Regina Lubala,Kange waeleza namna Kata zao zilivyojipanga kuhakikisha watoto wanapelekwa shule
*Muhula mpya wa masomo kuanza Januari 13,2026
Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Watendaji, wenyeviti, wazazi na walezi wilayani Ilemela mkoani Mwanza,wametakiwa kuhakikisha watoto wao wanaripoti shuleni kwa wakati pindi shule zinapofunguliwa Januari 13,2026 hata kama hana sare za shule.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Amir Mkalipa,wakati wa kikao cha Baraza la Ushauri la Wilaya (DCC) kilichofanyika Januari 8 2026, amesisitiza kuwa akisisitiza kuwa sare si kigezo cha kumnyima mtoto haki yake ya msingi ya kupata elimu.

Mkalipa amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bila vikwazo visivyo vya lazima, hususani kwa familia zenye changamoto za kiuchumi.
“Tunafungua shule tarehe 13 mwezi huu, kila Mwenyekiti na Mtendaji wa mtaa na kata ajiridhishe kuwa shule zake za msingi na sekondari ziko tayari kufunguliwa na kuhakikisha kila mtoto anaetakiwa kuripoti shule anafika,”amesema Mkalipa.
Sanjari na hayo amesema Serikali haitasita kumchukulia hatua mzazi asiyetaka kumpeleka mtoto wake shule kwa sababu yoyote ile.
Huku amewaonya walimu ambao ni wachelewaji na watoro kuwa watachukuliwa hatua bila kusita kwa mujibu wa sheria na kanuni, huku akiwataka Madiwani kuhakikisha shule zote zilizopo katika Halmashauri hiyo zinafunguliwa kwa wakati na wanafunzi wanapata haki yao ya elimu.
Wakizungumza na Timesmajira Madiwani wa Kata ya Pasiansi na Nyamanoro,wameeleza namna ambavyo wamejipanga kuhakikisha watoto waliopo katika maeneo yao wanaripoti shuleni kwa wakati pamoja na kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza.
Diwani wa Kata ya Pasiansi, Regina Lubala,amesema,katika Kata yake maandalizi ni mazuri na mwitikio wa kujindikisha watoto wanaonza awali na darasa la kwanza ni mkubwa.
Amesema wazazi wanaweza kukwamisha mtoto kuanza shule kutokana na kukosa sare za shule au madaftari.
“Tunafuatilia na siku mbili hadi wiki wakati wa kufungua shule,na utakuwa ni muda mzuri wa viongozi kuwafuatilia kuwa je,hao watoto wote walioandikishwa wamaehudhuria,kwa sababu katika Kata yangu tupo vizuri madawati ya kutosha yapo na tupo kwenye mchakato wa kukamilisha madarasa ambayo hayajakamilika katika shule ya msingi Jamhuri na Isenga ‘C’,lakini hayo siyo sababu ya kufanya wananfunzi wasiendelee na masomo,”amesema Regina.
Sanjari na hayo,Regina ametoa wito kwa wazazi na walimu kuwasaidia wanafunzi ili waweze kuingia katika masomo na wanapo kwama wawasiliane na viongozi kwa utatuzi zaidi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyamanoro,Abdulrahman Kange,amesema atawashirikisha Wenyeviti wa mitaa na wananchi kutoa elimu juu ya umuhimu wa watoto kwenda shule.
“Mwitikio wa uandikishaji kwa watoto wa darasa la kwanza mzuri,na tunaangalia ni changamoto gani zilizopo kwenye shule zetu ili kuzitatua na ifikapo Januari 13,2026 naamini muitikio utakuwa mkubwa wa wazazi kuwapeleka watoto shuleni,”amesema Kange.
Pia amesema elimu ni pembe tatu(triangle) kwa maana ya utatu ambao ni mtoto,mzazi na Mwalimu.
“Kwaio ninawasihi wazazi kwa sasa wanamuitikio mkubwa katika kuandikishwa watoto na kuwapeleka kuanza shule hivyo muitikio huo ufanyike katika kufuatilia masuala ya taaluma ya mtoto huku walimu watimize wajibu wao wa kuendelea kuwapa watoto elimu stahiki ya kuwasaidia kielimu,”amesema Kange na kuongeza:
“Na sisi tutaendelea kuboresha mahitaji yote yanayohitajika katika shule zetu na kupunguza changamoto walizonazo walimu ili kusiwe na sehemu ya kukwamisha utaratibu wa utoaji elimu kwa watoto wetu,”.
Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Nyamanoro Mashariki Kata ya Nyamanoro,Missa Budundu,kwa kushirikiana na walimu na wazazi watafanya kila watakaloweza kuhakikisha watoto wote wanaenda shule.
“Wazazi wawapeleke watoto shule kwani kwa sasa sera ya Serikali ni elimu bila malipo pia wawapeleke shule ambazo zipo karibu kuwasaidia watoto kuepuka na madhara ambayo yanaweza kujitokeza endapo zitakuwa mbali,”amesema Budundu.
Hata hivyo mmoja wa wakazi wa mtaa wa Nyamanoro Mashariki,Amina Kishogoto,amesema ameisha fanya maandalizi ya kuhakikisha watoto wake wamaehudhuria shule katika muhula mpya wa masomo kwani elimu ndio msingi na urithi bora kwa mtoto.
Muhula wa kwanza wa masomo kwa mwaka 2026 unatarajia kuanza rasmi Januari 13 kwa shule zote nchi nzima kufunguliwa.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi