March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mafundi mradi waujenzi wa madarasa,vyoo watakiwa kuzingatia ubora na muda

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online-Nkasi

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Peter Lijualikali, amewaagiza mafundi wanaotekeleza mirada ya ujenzi wa madarasa na vyoo katika shule za msingi Misunkumilo na Isunta kuzingatia muda na ubora ili kuendana na thamani ya fedha za Serikali.

Lijualikali ametoa agizo hilo katika ziara yake alipotembelea shule hizo ili kujionea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo.

Amesema serikali inatoa fedha nyingi ikukamilisha miradi mbalimbali katika sekta ya elimu, ili kuwezesha mazingira yenye ubora ya watoto kupata elimu.

Sambamba na hayo amewataka wataalamu na wasimamizi wa miradi hiyo kusimamia ipasavyo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati na inaendana na thamani ya fedha.

Katika hatua nyingine Lijualikali amewasisitiza walimu kutumia maeneo ya shule zao kulima mazao ya chakula kama mahindi ili wanafunzi wayatumie kwa chakula .

Hata hivyo amewaonya Walimu kutotumia sehemu kubwa ya maeneo ya shule kufanya shughuli za kilimo badala yake watumie eneo kubwa kwa ajili kulima mazao ya chakula kwa ajili ya wanafunzi.