Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online – Mwanza
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amesema Serikali inaendelea kutekeleza kwa vitendo mpango wa kuimarisha huduma ya maji nchini kuelekea kujenga gridi ya taifa ya maji itakayounganisha vyanzo mbalimbali vya maji ili kuwafikia wananchi moja kwa moja nyumbani.
Mhandisi Kundo,amezungumza hayo jijini Mwanza Januari 9,2026 wakati wa ziara ya kukagua mradi wa kuboresha huduma ya usambazaji wa maji ambao unajumlisha ujenzi wa matenki matano ya maji yenye uwezo wa lita za maji milioni 31 kwa siku pamoja na vituo viwili vya kusukuma maji.

“Nikirejea hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati akifungua Bunge, alisisitiza umuhimu wa kuwa na gridi ya taifa ya maji itakayochukua maji kutoka vyanzo mbalimbali kama Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika pamoja na mabwawa makubwa ikiwemo Kidunda na Nyumba ya Mungu, ili maji yawafikie wananchi moja kwa moja nyumbani,” amesema Mhandisi Kundo.
Ambapo ameeleza kuwa ujenzi wa matenki ya maji na vituo vya kusukuma maji unaotekelezwa Mwanza ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya maji yenye nguzo tatu kuu.
Mhandisi Kundo,amesema nguzo ya kwanza ya sera hiyo ni kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa kujenga vyanzo pamoja na vituo vya kusukuma maji ili maji yawepo. Nguzo ya pili ni kufikisha huduma hiyo kwa wananchi kwa kujenga miundombinu ya usambazaji ili kila mwananchi aweze kuunganishiwa maji hadi nyumbani.
Huku nguzo ya tatu ni kuhakikisha gharama za huduma zinaendana na uwezo wa wananchi pamoja na hali halisi ya uzalishaji wa maji.
“Maono ya Rais Samia ni kuona sera hii inatekelezwa kwa vitendo, ndiyo maana Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 46 za fedha za walipa kodi kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji Mwanza,” amesisitiza.
Pia amesema mradi huo hauongezi uzalishaji wa maji uliopo wa lita milioni 138 kwa siku,bali unaongeza uwezo wa kuyafikisha maji yaliyopo kwa wananchi ambao awali walikuwa hawapati huduma hiyo kutokana na jiografia ya jiji la Mwanza ambao ulisababisha gharama kubwa kwa kuwa na vituo vingi vya kusukuma maji(booster station.
“Maji yalikuwepo lakini hayakuwafikia wananchi. Mradi huu utawezesha maji kushuka kwa mserereko, hivyo kupunguza gharama za kuwa vituo vingi vya kusukuma maji.Mahitaji ya maji Mwanza ni lita milioni 180 kwa siku,uzalishaji wa sasa ni lita milioni 138 upungufu ni zaidi ya lita milioni 40,” amesema Mhandisi Kundo.
Hata hivyo ameeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo akisema tenki la Sahwa limefikia asilimia 78 ya ujenzi, huku kituo cha kusukuma maji kikiendelea vizuri.
“Kwa kasi niliyoiona na usimamizi mzuri wa MWAUWASA, nina imani mradi utakamilika kwa wakati na kutoa matokeo chanya kwa wananchi wa Jiji la Mwanza,” amesema.
Sanjari na hayo amesema,Serikali imejipanga kuendelea kuanzisha miradi mipya ya maji mara baada ya kukamilika kwa mradi huo hadi uzalishaji na mahitaji vitakapolingana.
“Mpango mkakati tayari upo, maandiko yanaandaliwa na usanifu kwa baadhi ya miradi umeanza,” amesema Mhandisi Kundo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Neli Msuya, amesema mradi huo unaendelea vizuri na umefikia asilimia 40 ya utekelezaji.
“Mradi ulianza Desemba 24, 2024 na unatarajiwa kukamilika Desemba 24, 2026. Vijana, wataalamu na vifaa vipo, na tuna uhakika utatekelezwa kwa ubora unaohitajika,” amesema Msuya.
Ameongeza kuwa matenki hayo yamejengwa juu ya vilele vya milima ili kupunguza gharama za usambazaji wa maji, huku yakilenga maeneo yenye changamoto kubwa ya maji na unatarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 450,000 wa Jiji la Mwanza.

Naye Mhandisi Mkazi wa mradi,Raphael Joseph, amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa matenki matano yenye ujazo wa lita milioni 31,ambayo ni Nyamazobe lita milioni 5,Buhongwa lita milioni 10, Kisesa lita milioni 5, Fumagila lita milioni 10 na Usagara lita milioni 1.
Ameeleza kuwa ujenzi huo unaambatana na ulazaji wa mabomba makuu yenye urefu wa kilomita 41 na ukubwa tofauti, pamoja na vituo viwili vya kusukuma maji vya Butimba na Sahwa.
“Mradi unagharimu takribani shilingi bilioni 46 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026,” amesema.



More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi