March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DKt.Homera kuongoza utoaji msaada wa kisheria Morogoro

*Huduma za haki kwa wananchi zinatolewa leo kupitia kliniki za msaada wa kisheria na ziara ya kikazi ya Wizara

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, anatarajiwa kuongoza zoezi la utoaji wa msaada wa kisheria bure mkoani Morogoro leo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara hiyo, wananchi wenye changamoto mbalimbali za kisheria wanahimizwa kujitokeza kupata huduma hizo bila malipo, hususani wanaokabiliwa na migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi, malezi na ulinzi wa watoto pamoja na upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa.

Huduma hizo zitatolewa kupitia kliniki maalum za msaada wa kisheria zitakazowahusisha wataalamu wa sheria na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria, ambapo wananchi watapatiwa elimu ya kisheria, ushauri wa kitaalamu na mwongozo wa hatua za kuchukua kulingana na changamoto zao.

Aidha, mkutano maalum wa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kwa pamoja unatarajiwa kufanyika katika viwanja vya stendi ya zamani Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, ambapo wananchi watapata fursa ya kuwasilisha kero na hoja zao moja kwa moja kwa wataalamu wa sheria na viongozi wa taasisi husika.

Mbali na utoaji wa huduma za msaada wa kisheria, Dkt. Homera anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi katika taasisi za haki zilizopo mkoani humo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu yao, kusikiliza changamoto zinazowakabili na kutoa maelekezo ya kuboresha huduma kwa wananchi.

Hatua hiyo inalenga kuisogeza huduma ya haki karibu na wananchi, hususani makundi yenye uhitaji wa msaada wa kisheria, sambamba na mkazo wa Serikali wa kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati, kwa usawa na bila vikwazo.

Ziara ya Waziri mkoani Morogoro ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi za Wizara ya Katiba na Sheria katika kuimarisha utawala wa sheria nchini, na inaaksi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha huduma za kisheria zinawafikia wananchi moja kwa moja walipo.