March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbaroni kwa tuhuma za kutupa kichanga juu ya paa

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

Jeshi la Polisi mkoani  Mwanza linamshikilia na linaendelea kumuhoji Fahima Twaibu (19) kwa tuhuma za kutupa kichanga, chenye jinsia ya kike, kinachokadiriwa kuwa na saa mbili tangu kuzaliwa.

Inadaiwa mtuhumiwa huyo ambaye ni mfanyakazi wa ndani na mkazi wa mtaa wa Balyehela, Kata na wilayani Ilemela  mkoani Mwanza,alitenda kosa hilo Desemba 25,2025 majira ya saa 11.00 alfajiri.

Akizungumza jijini hapa Desemba 29,2025,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbord Mutafungwa,amesema inadaiwa kuwa  Fahima alitupa kichanga hicho muda mfupi baada ya kujifungua kwenye paa la nyumba inayomilikiwa na Emmanuel  Murul, fundi wa kuchomelea vyuma na mkazi wa Balyehela.

Mutafungwa amesema,baada ya kupata taarifa Askari Polisi walifika eneo hilo na walifanikiwa kuokoa maisha ya kichanga hicho kwa kushirikiana Maofisa  Ustawi wa Jamii pamoja na wananchi wa eneo hilo.

Ambapo walikifikisha kichanga hicho hospitali ya Mkoa Sekou-Toure kwa matibabu huku uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Sanjari na hayo ametoa wito kwa jamii kushirikiana kwa karibu katika kulinda haki na maisha wa watoto kwa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi yao.

“Vitendo vya ukatili kwa watoto ni kosa la jinai na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivyo,”amesema Mutafungwa.