March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Milioni 485.7 yatolewa kwa vikundi 15 Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya 

*Patali aonya uchukuaji mali za wananchi wanaoshindwa kurejesha mikopo

*Asisitiza utoaji elimu kabla ya mikopo

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya 

Jumla ya mkopo wa shilingi  milioni 485.7 imetolewa kwa  vikundi 15 vya Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya huku onyo likitolewa kwa wenye tabia ya kuchukua mali za watu wanaoishindwa kurejesha mkopo husika.

Akikabidhi mkopo huo kwa vikundi hivyo mwishoni mwaka wiki kituo cha mabasi Tarafani Mamlaka ya Mji mdogo wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya Vijijini.  Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini,Patali Shida,amesema halmashauri hiyo imefanya vizuri kwa asilimia 60.

Huku akionya  tabia ya kuchukua mali za wananchi wanaoshindwa kurejesha mikopo huku akisisitiza  kuwa tafsiri yake inaonesha Maofisa Maendeleo ya Jamii hawakutoa elimu ya mikopo hiyo.

Shida amesema,ili kila mwananchi aweze kufahamu manufaa ya mikopo hiyo,ni wajibu wa Maofisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi.

“Maofisa maendeleo ya jamii kabla ya kutoa mikopo toeni elimu ili kusaidia wananchi kurejesha kwa wakati,kitendo cha kutumia dhamana kuchukua mali ni dalili za kutotekeleza majukumu yenu,”amesema Shida.

Sanjari  na hayo Patali,amewataka watendaji wa Serikali kuendelea kupambana kuongeza vyanzo na makusanyo ya mapato ya ndani ya halmashauri ili msimu ujao kuongeza idadi ya wanufaika wa mikopo hiyo ya asilimia 10.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mbeya, Abdul Yahaya,amesema katika kipindi cha miaka mitano jumla ya vikundi 356,vyenye sifa vilipata mkopo ambapo wanawake 175 ,vijana 163,na walemavu 19.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2020/2021 mpaka 2025/2026, halmashauri hiyo  imetoa mkopo wa zaidi ya bilioni 4.581 kwa vikundi 252 ikiwemo vya wanawake 114,vijana 126 na watu wenye  ulemavu vikundi 12.

“Jumla ya watu 3,345,kati ya hao 1,253, wanawake ,vijana 2,062 na watu wenye ulemavu 30 wamenufaika na mikopo asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri,”amesema Yahaya.