Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Tabora
ASKOFU wa Kanisa la TAG Jimbo la Tabora Kati na Kiongozi wa Kanisa la Kitete Christian Centre (KCC) la Mjini Tabora,Paul Meivukie ameomba upendo, haki na amani viendelee kudumishwa nchini ili jamii iishi kwa utulivu.
Ametoa rai hiyo kwenye ibada ya sikukuu ya Krismasi,ambapo ameeleza kuwa sikukuu hiyo ni tukio linalobeba ujumbe wa upendo, haki na amani kwa watu wote, hivyo mamlaka na jamii kwa ujumla hawana budi kuyadumisha.

“Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani,taifa liliingia kwenye wakati mgumu, hili halipaswi kufumbiwa macho.Kama taifa tunapaswa kusameheana na kupendana ili kudumishwa amani yetu,”amesema Askofu Meivukie.
Pia amewahasa waumini wa kanisa hilo na jamii kwa ujumla kuishi tabia na maisha ya Yesu Kristo na kuachana na njia zisizofaa ambazo husababisha chuki na uvunjifu wa amani.
Akinukuu maandiko kwenye kitabu cha Isaya 9:6 ameeleza kuwa “Mtoto Yesu alizaliwa kwa ajili yetu, ana uweza wa kifalme, ni mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele na Mfalme wa amani”.
Amesisitiza kuwa yeyote atakayemkubali Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake hatapotea kamwe, atakuwa salama na maisha yake hayatakuwa kama yalivyokuwa huko nyuma, atakuinua kiroho, kimwili na kiuchumi pia.

Askofu Meivukie amesisitiza kuwa Yesu Kristo ni zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa watu wote hapa duniani kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Luka Mtakatifu 2: 10-11,”maana katika Mji wa Daudi amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi