Na Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Kilimo Japhet Hasunga ameipongeza kampuni ya usambazaji zana za kilimo ya Agricom Africa kwa kutumia vijana wa Tanzania kutengeneza matela ya trekta kwa gharama nafuu ukilinganisha na zile za kuagiza nje.
Akizungumza katika hafla ya utilianaji saini mkataba kati ya Benki ya CRDB na kampuni tatu za usambazaji wa zana za kilimo jana, Waziri Hasunga amesema Agricom Africa imekuwa ikitekeleza kwa vitendo azma ya serikali ya ujenzi wa viwanda kwa kuwaamini vijana na kuwatumia kufanya uzalishaji.
“Kilimo ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya viwanda na pia kilimo kimekuwa kinatoa mchango wa asilimia 28 ya pato la taifa. Naipongeza sana Agricom Africa kwa kuona hilo na kuanzisha teknolojia ya utengenezaji wa matela ya trekta hapa nchini,’’ amesema Hasunga.
Alisema teknolojia hiyo mbali ya kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda nchini, pia itachangia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya ajira kwa vijana wa Tanzania pamoja na kukuza uchumi wananchi kwa ujumla.
“Dira ya Taifa ya maendeleo 2025 na mpango wa pili wa Taifa wa maendeleo vimeweka mkazo kwenye mapinduzi ya viwanda na tunapowaona Watanzania wazalendo wanafanya mageuzi hayo inakuwa ni jambo la kupongezwa kwa kuwa wanaelewa serikali inasimamia wapi na wao wafanye nini,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Agricom Africa, Angelina Ngalula, alisema wataendelea kutumia fursa zilizopo kuhakikisha sekta za viwanda na kilimo inaongeza tija katika uchumi wa Taifa kwa kuwafanya wakulima nchini waendeshe kilimo cha kisasa.
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa kuweka mazingira rafiki kwa watu wa sekta binafsi kuwekeza katika miradi mabalimbali. Tutatumia mazingira hayo kuhakikisha tunatoa mchango stahiki ili kufikia malengo ya nchi iliyojiwekea,” amesema Ngalula.
Alisema teknolojia hiyo ya utengenezaji wa metela ya trekta utasaidia sana kupunguza gharama kwa kampuni yake kwani kampuni imekuwa ikiagiza matela kutoka nje ya nchi.
“Tumekuwa tukiagiza matela hayo kutoka nje ya nchi kwa gharama lakini sasa tunatengeneza hapa nchini kupitia vijana wa kitanzania kwa gharama ya milioni 2.4 jambo ambalo limepunguza gharama hizo maradufu na pia muda wa upatikanaji wake umepungua,’’ ameeleza Ngalula.
Mwidini Mwidin mmoja wa wanufaika wa mkopo wa kupata trekta mbali ya kuipongeza Agricom, alisema atatumia trekta hiyo kujiimarisha katika kilimo kwani ni sekta inayochangia upatikanaji wa chakula kwa asilimia 100 imekuwa chanzo muhimu cha upatikanji wa malighafi ya viwanda.
Mwishoooooooo
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea