March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa dini Kagera waomba mijadala ya mara kwa mara

Na Mwandishi wetu Timesmajira Online- Bukoba,

Serikali mkoani Kagera imeombwa kuwa inakutana na viongozi mbalimbali wa dini na kwa kufanya nao mijadala ya mara kwa mara ya kuona namna bora ya kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza na kusababisha uvunjifu wa amani ambayo ni tunu ya taifa.

Maombi hayo yametolewa leo na viongozi wa dini wakati wa dua na sala ya kuombea taifa na Mkoa huo katika uzinduzi wa kongamano la Ijuka Omuka (kumbuka nyumbani)lililoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Hajat Fatma Mwassa kwa lengo la kutangaza fursa za kiuchumi zilizipo mkoani humo.

Shekh Abdulshahid Abbas ni kiongozi wa Answari Suna,amesema viongozi wa dini wamepewa dhamana ya kuhakikisha watu wanakwenda mbinguni na siyo motoni. Mwalimu mzuri ni yule anayefundisha wanafunzi wake kulinda amani ya nchi yao pia wazazi wazuri ni wale wasiosahau wajibu wao wa malezi kwa watoto.

Shekhe Abbas,amesema vitabu vyote vya dini vinahimiza watu kuwa wamoja,kupendana ,kupenda nchi zao na kuto hasi mema tunayojaaliwa na Mungu,maana hakuna shetani mbaya kama mtu anayehimiza mihemko kwa vijana eti ‘Gen-z’waende kuharibu rasilimali za nchi yao kutokana na uchochezi wa watu wabaya wasiotutakia mema.

“Nawashauri viongozi wa serikali kuweka utaratibu wa kutuita na kukaa pamoja mara kwa mara,ili kuweka mambo sawa ambayo yanatatiza watu wetu kabla hayajaleta madhara yanayoweza kuliangamiza taifa letu.Silaha kubwa ya kumaliza mambo pindi kunapokuwa ns taharuki ni vyema kunyamza na kumuomba Mungu kwani hiyo ndiyo busara,”amesema.

Padre Philibart Mutalemwa Mkuu wa Idara ya Utume na Walei Jimbo katoriki la Bukoba na Mchungaji Ayub Silvester wa madhehebu ya CPCT wamewaomba wanakagera na watanzania kulinda amani ya nchi,kuondokana na moyo wa kubaguana kwa njia yoyote ikowemo udini,ukabila na jinsia bali wapendane na kuheshimiana pia wasiruhusu watu kuwachonganisha kwa njia yoyote.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajat Fatma Mwassa, amesema wanakagera waliisha onja machungu ya uvunjifu wa amani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vita ya Kagera ya mwaka 1978 na matukio mengine kama vile ugonjwa wa upungufu wa kinga mwilini ( Ukimwi ).

Pia ajali ya meli ya Mv.Bukoba na ndege zilizochukua maisha ya watu wengi hali ambayo ilirudisha maendeleo ya Mkoa huo nyuma hivyo waliona ni vyema kujiepusha na uvunjifu wa amani hivyo amewashukuru na kuwapongeza.

Hata hivyo amewaomba wananchi kuendelea kuilinda amani ya Mkoa wa Kagera kwa maslahi ya taifa na vizazi vyao kwa kuendelea kuwa wazalendo.