March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MECIRA yatoa wito kwa watanzania kuendelea kulinda amani

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online-Dar

KITUO cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA) kimetoa wito kwa Watanzania kuendelea kulinda amani, mshikamano wa kitaifa na maelewano ya kidini, huku kikisisitiza umuhimu wa kuepuka kuruhusu kutumiwa au kushawishiwa kujiingiza katika mipango ya vurugu na machafuko.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-es-Salaam, Mwenyekiti wa MECIRA, Habibu Mchange, amesema kituo hicho kimeanza kuchukua hatua za kuziarifu nchi za Marekani na Kenya kuhusu kile alichokitaja kuwa ni jitihada za kuhamasisha vurugu, machafuko na kusambaza taarifa potofu dhidi ya Tanzania kupitia nchi zao.

” Tumechukua hatua kuuarifu Ubalozi wa Marekani na Ubalozi wa Kenya nchini Tanzania kuhusu kuendelea kukua kwa vitendo vya uhamasishaji wa vurugu na machafuko,chuki za kijamii na kuhatarisha usalama wa Taifa kupitia mitandao ya kijamii kinachofanywa na baadhi ya watanzania na wasio watanzania wanaoishi katika nchi zao,”amesema Mchange.

Amesema katika barua hizo wameweka bayana kuwa wanatambua na kuheshimu taifa la Marekani linalojengwa juu ya misingi ya demokrasia,haki za binadamu na uhuru wa kujieleza

Aidha amevitaka vyombo vya habari, wanaharakati pamoja na viongozi wa jamii kutumia uhuru wao kuwajibika, kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa na kuepuka kuchochea migawanyiko au machafuko katika jamii.

Pia ametumia fursa hiyo kuwatahadharisha vijana kuwa kushiriki katika uhamasishaji wa machafuko kunaweza kuwasababishia madhara ya kisheria, kijamii na kifamilia, hivyo amewataka kuwa makini na jumbe au vishawishi wanavyokutana navyo, hususani kupitia mitandao ya kijamii.

“MECIRA inasiitiza kuwa amani ya Tanzania si ya kujadiliwa, na mtu yeyote anayehubiri, kupanga au kuratibu machafuko yanayosababisha kupotea kwa maisha ya watu anapaswa kuwajibishwa kisheria kwa tuhuma za kusababisha vifo, bila kujali yuko wapi au anatumia jukwaa lipi,”amesema Mchange

Ameongeza kuwa kituo hicho kitaendelea kutumia njia za kiraia, kidiplomasia na kisheria kuhakikisha Tanzania inalindwa dhidi ya vurugu, propaganda hatarishi na migawanyiko ya kijamii.

Sanjari na hayo ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuheshimu uhuru wa ndani, mamlaka ya kikatiba na mshikamano wa kijamii wa Tanzania, na kutochanganya au kuhalalisha uhamasishaji wa vurugu kwa kisingizio cha haki za binadamu au uhuru wa kujieleza.

Amesema ni muhimu kutumia taarifa zilizothibitishwa na zenye mizani, badala ya zile zinazopandikiza chuki za kidini, kikabila au kisiasa, .

Ameongeza kuwa uwamasishaji unaosababisha vifo si hoja ya kisiasa bali ni uhalifu unaopaswa kushughulikiwa kisheria.