Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
SERIKALI ya Tanzania imethibitisha kuendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika huduma za mawasiliano.
Lakini pia, ikitambua mchango muhimu wa Kampuni ya Mawasiliano Yas katika kuendeleza mabadiliko ya kidijitali nchini.
Akizungumza katika ziara yake ya kikazi hivi karibuni katika makao makuu ya Yas, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki (Mb), ameipongeza kampuni hiyo kwa mchango wake mkubwa katika kuchochea mapinduzi ya kidijitali

Amesema, hususan katika miamala ya kifedha, upanuzi wa mawasiliano vijijini, uwekezaji katika miundombinu, na ajira zinazotolewa kwa Watanzania.
Waziri Kairuki ameishukuru Yas kwa kuwekeza USD milioni 47.6 katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) ndani ya miaka mitatu, sambamba na ushirikiano wake na Serikali katika ujenzi wa minara 560 ya mawasiliano, miradi ambayo imekamilika kwa wakati.
“Yas ina wajibu wa kuendelea kuwaunganisha wananchi na huduma za mawasiliano, hasa wale vijijini, bila kumwacha mtu yeyote nyuma wakiwemo wanawake, watu wenye ulemavu, na makundi mengine yaliyo pembezoni,” alisema Waziri Kairuki.
Aidha, ameitaka kampuni kuongeza uwekezaji katika miamala ya kifedha, kuhakikisha faragha na usalama wa taarifa za wateja, na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu huduma zao.
Pia, amehimiza Yas kuendeleza ujuzi wa wafanyakazi wake kupitia mafunzo ya mara kwa mara ili waendane na mabadiliko ya teknolojia.

Waziri Kairuki pia emeipongeza Yas kwa kutoa mafunzo kwa vijana takribani 9,000, akiwataka kuongeza juhudi za kuwawezesha vijana, hasa wasichana, katika ujuzi wa TEHAMA.
“Kwa upande wetu, tutaendelea kujenga mazingira wezeshi ili muone matunda ya vijana mnaowawezesha,” alisema.
Aidha, amethibitisha kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kuandaa sera zinazowezesha kampuni kama Yas kukua kibiashara, kulinda maslahi ya watumiaji, na kuimarisha uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas, Pierre Canton Bacara, amesema wao kama mshirika wa kidijitali wa Watanzania, Yas imejidhatiti katika kupanua upatikanaji wa huduma zinazochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa.
“Kupitia uwekezaji wetu, tunalenga kuwaunganisha Watanzania, kupunguza pengo la huduma kidijitali, na kusaidia Serikali kuijenga Tanzania yenye ujumuishi katika masuala ya kifedha, ubunifu, na teknolojia,” amesema.


More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani