September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Failuna, Geay kukiwasha World Half Marathon

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

NYOTA wa timu ya Taifa ya Riadha Failuna Abdi na Gabriel Geay wataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Dunia ya riadha ya ‘World Half Marathon’ yatakayofanyika Oktoba 17, Gdynia nchini Poland.

Kuelekea katika mashindano hayo, tayari usajili wa kwanza umeshakamilika na kinachosubiriwa ni usajili wa mwisho utakaofanyika Septemba 28.

Nyota hao watakwenda kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo huku wakiwa wametoka kufanya vizuri katika mashindano ya mbio za Ngorongoro yaliyofanyika juzi.

Katika mashindano hayo Geay aliibuka kinara kwa upande wa wanaume akitumia saa 1: 4 : 42 na kuvunja rekodi iliyowekwa mwaka jana na Abraham Too kutoka Kenya, aliyetumia saa 1: 5: 59 na kumshinda Herman Sule kutoka Mbulu aliyetumia 1: 6: 10 na Josephat Joshua kutoka Polisi Tanzania aliyetumia saa 1: 6: 57.

Kwa upande wa wanawake, mshindi wa jumla alikuwa Failuna kutoka klabu ya Talent ya Arusha aliyetumia saa 1: 16: 3 akimpuki mshindi wa mwaka jana Esther Chesang kutoka Kenya aliyetumia saa 1:16:49 huku nafasi ya pili Natalia Sule kutoka klabu hiyo akitumia saa 1:16:43.

Ushindi wa nyota hao umewafanya kuvunja rekodi zilizowekwa mwaka jana na Wakenya ambao hawakuweza kushiriki kutokana na Covid-19.

Kocha wa wanariadha hao, Thomas Tlanka ameuambia Mtandao huu kuwa, wanariadha wake wapo fiti kushiriki mashindano hayo kwani kiwango walichokionesha katika mashindano ya ngorongoro kinawapa imani ya kurudi na medali hapa nchini.

Amesema, hadi sasa tayari usajili wa awali umeshakamilika na wanachokisubiri ni usajili ya mwisho utakaofanyika Septemba 28 na kusubiri kutumiwa tiketi.

“Failuna na Geay watashiriki mashindano ya World Half Marathon na tunaimani kubwa kuwa wataweza kufanya vizuri na kurudi nchini na medali kutokana na kiwango chao kuendelea kuwa bora, ” amesema kocha huyo.

Hata hivyo amewaomba wadau mbalimbali wa riadha ikiwemo mashirika kuwasaidia katika maandalizi ya mwisho ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano hayo.

“Kwa kuwa mashindano haya ni makubwa tunaomba sapoti kutoka serikalini, mashirika ya umma na binafsi ili kuweza kuwapa hamasa ya kufanya vizuri zaidi na kurudi na medali,” amesema kocha huyo.

Kwa upande wake Msemaji wa Shirikisho la Riadha nchini (RT), Tullo Chambo amesema kuwa, tayari wameshaanza mchakato wa kuwaombea visa wanariadha hao wanaotarajiwa kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo makubwa duniani yatakayofanyikia Poland.

Amesema, wanaamini kuwa kiwango kilichooneshwa na Geay katika mashindano ya riadha ya Taifa pamoja na Ngorongoro ambayo pia Failuna aliibuka kidedea kitawapa matokeo mazuri.

Tullo amesema kuwa, pia anaungana na kocha wa wanariadha hao kuwaomba wadau kuwaunga mkono katika maandalizi yao ya mwisho ili kuwaongezea hamasa ya kupambana na kufanya vizuri na kurudi nyumbani na medali.