*Lengo ni kuimarisha usalama barabarani hasa kipindi hiki cha sikukuu
*Kuhimiza matumizi ya tiketi mtandao zenye viwango halisi vya nauli
Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA), Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamezindua kampeni ya “Abiria Paza Sauti” katika kituo cha mabasi cha Nyamh’ongolo wilayani Ilemela mkoani hapa.
Kampeni hiyo ikiwa ni jitihada za kulinda haki za wasafiri na kuimarisha usalama barabarani wakati wa msimu wa sikukuu huku ikilenga kuwajengea uelewa mpana abiria kuhusu wajibu na haki wanapotumia usafiri wa barabara.

Pamoja na kuhimiza matumizi ya tiketi za mtandao zenye viwango halisi vya nauli vilivyo ainishwa na serikali kupitia LATRA.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Desemba 6,2025,Katibu wa RSA Mkoa wa Mwanza, Subra Sabi, alisema kampeni hiyo ni jukwaa la kuwaelimisha abiria umuhimu wa kutoa taarifa, malalamiko na kerowanazokutana nazo wakiwa safarini.
Ikiwemo uvunjifu wa sheria za usalama barabarani, uongezaji wa nauli kinyume cha taratibu, kupakia mizigo kupita kiasi au matendo mengine yanayotishia usalama na ustawi wao.
“Serikali imeweka miongozo na mifumo ya kutoa taarifa na sisi tunahimiza watu kuitumia fursa hiyo.Hii ni kampeni ya kuwatia nguvu abiria kipindi hiki cha likizo na msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka na mkwanzo wa mwaka. Tunataka wapaze sauti zao bila woga pale wanapofanyiwa vitendo visivyoendana na sheria,” alisema Subira.
Subira alisisitiza kuwa kupitia kampeni hiyo abiria wapaze sauti kukomesha tabia ya kushushwa ama kupandishwa katika magari yasiyofaa kisheria, kutozwa nauli isiyozingatia umbali, madereva kuendesha mwendokasi na makosa mengine ya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.
Mratibu wa RSA Kanda ya Ziwa, Abdulaziz Bangu,alisema, kampeni ya Abiria Paza Sauti ni mkakati unaolenga kupunguza ajali za barabarani baada ya abiria kutoa kero na malalamiko yao kwa mamlaka na kuchukua hatua.
“Tunafanya hivi kuwapa abiria uelewa na kueleza kero za uvunjifu wa sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali.Uzoefu unaonesha mwisho wa mwaka na mwanzoni ajali nyingi za barabarani hutokea, inatokana na wingi wa watu kusafiri na hivyo wamiliki wasio waaminifu hutumia fursa hiyo kuingiza magari yasiyostahili,”alisema Bangu.

Naye Sajenti Veronica Pamba wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, alisema abiria wanatakiwa kuzifahamu namba za simu za taasisi hiyo, milango ya dharura ya kujiokoa wakati wa ajali na kila gari liwe na mtungi wa kuzima moto.
Kwa upande wake Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA), Mkoa wa Mwanza, Steven Kusupa, mbali na kuweleza abiria na wadau wa usafiri na usafirishaji majukumu ya taasisi hiyo, alisema wanaangalia mazingira ya usafirishaji na kuhakikisha abiria wanatendewa haki.
“Tiketi mtandao lazima iwe na jina la abiria, namba yake ya simu, namba ya chombo na jina, kiwango cha nauli aliyolipa na mahali anapoishia.Pia majukumu yetu ni kutoa lesseni kwa vyombo vya usafirishaji,kupanga nauli, kuuhisha leseni na kuzuia magari yanayokiuka sheria,”alisema Kusupa.

Naye Stesheni Sajenti wa Polisi, Edna Kisanko alisema kupitia kampeni ya Abiria Paza Sauti, wanawakumbusha abiria haki zao wakiwa safarini katika vyombo vya usafiri na madereva kuzingatia sheria za usalama barabaran ili kuepuka ajali.
“Lengo abiria wakipata changamoto wakiwa ndani ya magari wafahamu haki zao pia watambue haki ni kwa pande zote kwa maana mtoa huduma na mpokea huduma.Pia, tunawakumbusha madereva kipindi hiki cha sikukuu wazingatie sheria za usalama barabarani,”alisema Kisanko.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako