March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Brigedia Jenerali Itang’are afunga rasmi mafunzo ya washiriki 48 ya Afya ya Akili na Msaada wa Kisaikolojia

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

KAMANDA wa Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are, amefunga rasmi Mafunzo ya Afya ya Akili na Msaada wa Kisaikolojia (MHPSS) pamoja na Kozi ya Usimamizi wa Usafirishaji (Logistics )katika misheni ya Ulinzi wa Amani kwa watendaji wa Umoja wa Mataifa, Awamu ya 02/25.

Akizungumza jana wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo, Brigedia Itang’are aliwapongeza washiriki wote kwa kujituma, nidhamu na ushiriki wao wa kina katika kipindi chote cha mafunzo ambapo kozi hiyo imeendeshwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya United Nations Institute for Training and Research (UNITAR).

Amesema takribani washiriki 48 wamehitimu mafunzo hayo ambapo kwa kozi ya MHPSS washiriki 19 wameshiriki mafunzo hayo na kwa kozi ya Logistics walikuwa washiriki 29.

“Kozi zote mbili ni muhimu sana kwa wananchi wetu hususan katika misheni za ulinzi wa amani kwani wote tunaelewa mafanikio yoyote katika operation ya kijeshi yanatakiwa kuwa logisc iliyokamilika.

“Maofisa hawa walipata mafunzo mazuri ambayo yatawawezesha kuingia katika mifumo ya utendaji katika Idara ya logistics katika umoja wa Mataifa na vilevile itawawezesha kufanya kazi katika misheni nyingine,”amesema.

Aidha Brigedia Itang’are amesisitiza kuwa afya ya akili na uimara wa kisaikolojia ni nguzo muhimu katika operesheni za ulinzi wa amani, hasa katika mazingira ya sasa yenye changamoto nyingi na misukosuko ya kiutendaji.

Amesema kuwa ujuzi na maarifa waliyopata haupaswi kubaki katika nadharia pekee, bali yanapaswa kutumika kwa vitendo katika majukumu yao ya kila siku. “Nawahimiza wahitimu kuwa mabalozi wa ustawi wa kisaikolojia katika vikosi vyenu na kuwasaidia wenzenu wanaoweza kukumbana na changamoto za kiakili au kihisia katika maeneo ya operesheni,”amesema.

Brigedia Jenerali Itang’are pia amebainisha kuwa Umoja wa Mataifa unatambua kwa kiwango kikubwa umuhimu wa afya ya akili kama uti wa mgongo wa utayari wa kiutendaji, mafanikio ya misheni na kulinda utu wa binadamu.

Amewasisitizia washiriki kudumisha viwango vya juu vya weledi, huruma na uadilifu wanapotekeleza kanuni za MHPSS katika majukumu yao.

Akihitimisha, ameonyesha imani kuwa Awamu ya 02/25 itatoa mchango mkubwa katika kuboresha ustawi, uimara na utendaji wa walinda amani wanaohudumu katika maeneo mbalimbali duniani.