March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB yajipanga kuinua kilimo biashara Kanda ya Ziwa

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB),imejipanga kuwasaidia wakulima nchini kutoka kwenye kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha biashara pamoja na kuhakikisha nchi inakuwa na usalama na utoshelevu wa chakula.

Hayo yameelezwa Desemba 3,2025 na Meneja wa TADB Kanda ya Ziwa,Alphonce Mokok,katika warsha ya siku mbili ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza iliondaliwa na benki hiyo na kufanyika jijini Mwanza.

Mokik amesema,dhamira ya benki hiyo ni kuchochea mageuzi ya kilimo kupitia suluhu za kibunifu za mikopo ili kuendeleza minyororo ya thamani ya kilimo endelevu na shirikishi pamoja na kuchangiza ukuaji wa uchumi ,usalama wa chakula na kupunguza umaskini.

Amesema Kanda ya Ziwa ni kitovu cha uzalishaji nchini ambako kwa sehemu kubwa yanapatikana mazao ya kimkakati kama pamba,kahawa, mpunga,mahindi,mbaazi,maharage pamoja na ufugaji wa samaki,ng’ombe na kuku.

Hivyo kwa kutambua umuhimu huo TADB,imejipanga kuhakikisha rasilimali za kifedha zinamfikia mkulima wa Kanda ya Ziwa kwa wakati na kwa ufanisi.

Pia amesema yapo mafanikio kwa upande wa Kanda ya Ziwa ambayo yamepatikana baada ya benki hiyo kuanzishwa mwaka 2012 chini ya Sheria ya makampuni no.2 ya mwaka 2002,baada ya sera ya kilimo kwanza na kuanza kufanya kazi rasmi mwaka 2015.

Ambapo imeisha toa mikopo takribani bilioni 631.18 katika miradi 151 kwa Kanda ya Ziwa huku kwa Mkoa wa Mwanza peeke imeisha toa jumla ya bilioni 79.14 kwa miradi 61.

Pia amesema,benki hiyo imefanikiwa kuendeleza kilimo cha mazao ya kimkakati ambapo imewezesha ufufuaji wa viwanda vinne vya kuchataka pamba vinavyomilikiwa na vyama vya ushirika.

“Ambapo tumeisha toa mikopo ya bilioni 171.58 hadi kufikia Oktoba mwaka huu,pia bei ya pamba mbegu imekuwa kutoka shilingi 900 kwa kilo mpaka shilingi 1,500,”amesema Mokik.

Aidha imewezesha kuchangiza upatikanaji wa masoko,kuboresha uzalishaji, kuongeza thamani kwa zao la kahawa ambapo bei kahawa ya maganda imekua mpaka kufikia shilingi 5,000 kwa kilo moja.

“Tumefadhili upanuzi wa miundombinu ya uhifadhi,ununuzi wa mitambo ya kukoboa na kukausha mazao na mikopo ya pembejeo kwa wakulima wadogo ambapo jumla ya bilioni 55.89 imetolewa,”amesema Mokik.

Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda,amewataka vijana pamoja na waandishi wa habari kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na TADB, ili kujikwamua kiuchumi.

Mtanda,amesema katika kipindi cha mwaka 2024/25 jumla ya bilioni 7.5 zimetolewa kwa vijana kama mkopo usio na riba na benki ya TADB kwa vijana 350 wanaofanya shughuli za uvuvi wa kisasa wa kutumia vizimba walio katika vikundi 47.

Ambapo vijana hao wameanza kupata faida na kurejesha shilingi bilioni 1.3 kwa awamu ya kwanza.