March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau watoa vifaa tiba wodi ya mama na mtoto Mnazi Mmoja

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar

Wodi ya mama na mtoto ya hospitali ya Mnazi Mmoja jijini Dar-es-Salaam imepatiwa vifaa tiba na wadau ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini.

Vifaa hivyo vimetolewa na taasisi ya Seris Foundation inayojishughulisha na vijana wa fani za sayansi na teknolojia pamoja na malezi ya watoto wachanga kuanzia siku ya kuzaliwa hadi miezi mitatu, kwa kushirikiana na Klabu ya Lions International.

Akizung;pumza wakati wa kukabidhi msaada huo,jijini Dar-es-Salaam,Desemba 1,2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Seris Foundation,CPA Deborah Wami, amesema malengo ya taasisi hiyo ni kufika kwa jamii na kugusa maisha ya watoto wachanga pamoja na akina mama wanaohudumiwa hospitalini.

Amesema msaada huo unajumuisha sare 50 za wagonjwa, taulo 50 za watoto, kofia 50, soksi 50, pamoja na magauni 50 kwa ajili ya akina mama wanaojifungua, vifaa ambavyo vitaisaidia hospitali hiyo kukidhi mahitaji ya wodi ya mama na mtoto.

“Leo tumefika kuangalia hali ya mama na mtoto mchanga aliyezaliwa, hususani wale walio chini ya miezi mitatu. Tumekuja kuwaona na kuwafariji, tukiamini kuwa matendo mema ndiyo yanayotakiwa katika vitabu vya imani,” amesema CPA Wami.

Amesema,hospitali ya Mnazi Mmoja ni miongoni mwa vituo vinavyokabiliwa na mahitaji kutokana na eneo lake katikati ya jiji, hivyo taasisi imeona umuhimu wa kuanza kusaidia hapo kutokana na ukaribu wake na ofisi zao.

Pia amewahimiza wadau wengine kutembelea hospitali na kutoa misaada kwa watoto wachanga na akina mama, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni njia ya kugusa jamii moja kwa moja.

Kwa upande wake, Gavana Bakari Omary kutoka Lions Club International,amesema wameunganisha nguvu na Seris ili kuongeza thamani ya msaada kwa jamii.

“Kama Watanzania sisi ni familia moja. Matatizo yaliyopo ndani yetu ni lazima tuyatatue kwa pamoja. Serikali inajitahidi, lakini ni wajibu wa watu binafsi na mashirika kuongeza nguvu ili jamii inufaike zaidi,” amesema Gavana Omary.

Aidha ametoa wito kwa mashirika binafsi na yasiyo ya kiserikali kuelekeza nguvu zaidi katika huduma za kijamii, hususani maeneo yanayohusu ustawi wa mama na mtoto.

Naye Muuguzi Kiongozi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Shufaa Kaniki ameishukuru Seris Foundation pamoja na Lions Klabu kwa msaada huo, akisema umefika wakati muhimu ambapo hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa za vifaa.

“Wamechagua eneo la mama na mtoto kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kuboresha sekta ya afya. Tunawashukuru kwa moyo waliouonesha na kutujumuisha kama sehemu ya jamii wanayoihudumia,”.