March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jeshi la Polisi Mwanza laendesha msako maeneo ya milimani na mapango

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeendesha operesheni maalumu ya msako na doria katika maeneo ya milima na mapango yanayotajwa kuwa maficho ya wahalifu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutokomeza uhalifu mkoani humo.

Akizungumza wakati wa doria hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP.Wilbrod Mutafungwa,alisema operesheni hiyo ilianza rasmi Novemba 29,2025, ikihusisha maeneo ya Kata za Mkolani, Buhongwa, Isamilo, Mhandu, Igoma Kati na Mahina wilaya ya Nyamagana.

Huku kwa Wilaya ya Ilemela  ilihusisha maeneo ya Kitangiri, Bwiru Ziwani, Kawekamo na Ibungilo.

“Tumekuwa tukipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu wahalifu wanaojificha katika mapango na maeneo ya milimani,wakijiandaa kutekeleza matukio ya uhalifu, hasa kuelekea mwishoni mwa mwaka. Hii imetulazimu kuchukua hatua za haraka,” alisema DCP.Mutafungwa.

DCP. Mutafungwa,alisema jumla ya watuhumiwa 12 wamekamatwa wakiwa wamejificha katika mapango hayo huku wakiwa na vifurushi vya bangi na kuongeza kuwa wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria baada ya upelelezi kukamilika.

Alisema,operesheni hiyo ni endelevu na Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha ulinzi na usalama vinadumishwa mkoani Mwanza.

Katika hatua nyingine,DCP. Mutafungwa ametoa wito kwa wakazi wa maeneo ya milimani, misituni na jirani na mapango kutoa taarifa mapema endapo watabaini uwepo wa watu wasiowafahamu au wanyama wakali ili hatua zichukuliwe mara moja.

Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kasese, Gaudence Mtepa,aliliomba Jeshi la Polisi kusaidia kulipua baadhi ya maeneo ya milima yanayotumika mara kwa mara na wahalifu kama maficho baada ya kutekeleza matukio ya uhalifu katika mitaa jirani.

“Jeshi la Polisi limefanya jambo la muhimu kukagua mazingira ya milima na mapango na kuona usalama wa mazingira yetu yanakuaje,”alisema Athanas Mwagama mkazi wa Mkolani.