Na Joyce Kasiki,Dodoma



SERIKALI imetenga zaidi ya shilingi trilioni moja katika zabuni za umma kwa ajili ya kuwezesha makundi maalum kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kujikomboa kiuchumi.
Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Remija Salvatory, alitoa taarifa hiyo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Kongamano la Ujumuishaji wa Watu Wenye Ulemavu kwenye Fursa za Kiuchumi.
Alisema lengo la kongamano hilo ni kuwawezesha watu wenye ulemavu kutambua na kunufaika na nafasi zilizopo katika ununuzi wa umma.
“Serikali imetenga asilimia 30 ya tenda zake kwa ajili ya makundi maalum, hivyo watu wenye ulemavu wana fursa kubwa ya kupata zabuni hizo. Kama PPRA tumekuja kuwaeleza kuwa serikali ya awamu ya sita inawathamini na kuwajali,” alisema Remija.
Amefafanua kuwa zabuni zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni moja zimetengwa kupitia taasisi za serikali, huku kila taasisi ikitakiwa kutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi kwa makundi maalum.
“Hivyo taasisi zote zimeelekezwa kufanya hivyo. Tumekuja kutoa hamasa na elimu kuhusu uwepo wa fursa hizi,” aliongeza.
Aidha, alisema mpaka sasa zabuni zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 24 zimetolewa mahsusi kwa makundi maalum.
Hata hivyo, alibainisha kuwa ni makundi takribani 1,000 pekee ndio yamejisajili, idadi ambayo ni ndogo ukilinganisha na wigo wa fursa zilizopo. Amewahimiza watu wenye ulemavu kujiunga katika vikundi vya watu 5 hadi 20 ili kutambuliwa na halmashauri na kupata nafasi ya kushindania zabuni kupitia mfumo wa NeST.
Wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Bruno Mwakibibi, alitoa wito kwa halmashauri kukusanya taarifa na takwimu za watu wenye ulemavu ili kuwaingiza katika mfumo wa utambuzi utakaorahisisha utoaji wa huduma.
Amewataka viongozi wa serikali za mitaa kuendelea kuwaibua, kuwasajili na kuwahusisha kikamilifu watu wenye ulemavu katika shughuli za ujenzi wa taifa.
Kwa upande wake, Katibu wa SHIVYAWATA Mkoa wa Dodoma, Justus Ng’antalima, alisema kongamano hilo litawafungua macho wajasiriamali wenye ulemavu kuhusu namna ya kuzitumia fursa za kiuchumi zinazowazunguka.
“Pia litawasaidia kuelewa huduma zinazohitajika na serikali ili waweze kushindania zabuni kupitia mfumo wa kielektroniki wa NeST,” alisema.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina