Na Mwandishi Wetu, Timesmajira online
Benki ya Absa imeibuka mshindi wa tuzo ya “Benki Inayopendekezwa na Kufikiwa zaidi Mashariki na Kusini mwa Afrika” katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Chaguo la Walaji 2025 iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Uendeshaji wa Matawi wa Benki ya Absa Tanzania, Irene Mwilongo, amepokea tuzo hiyo kwa niaba ya benki, akiwa pamoja na baadhi ya wafanyakazi wenzake ambao walishiriki kwenye hafla hiyo kama sehemu ya timu iliyochangia mafanikio hayo.
Katika tukio hilo, Mwilongo pamoja na timu yake walionekana wakiionesha tuzo hiyo mara baada ya kukabidhiwa, ishara ya furaha na uthibitisho wa namna wateja wanavyoitambua Absa kama benki inayoaminika, inayofikiwa kwa urahisi na kupendekezwa na walaji katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Akimkabidhi tuzo hiyo, mwakilishi wa waandaaji wa tuzo za Chaguo la Walaji, Balqis Njuki, ameipongeza Absa kwa kuendelea kuboresha huduma, kuwekeza katika ubunifu na kuhakikisha huduma za kifedha zinafika kwa wateja wengi zaidi.

Naye Mkuu wa Uchambuzi wa Utendaji wa Biashara wa Absa Tanzania, Stivia Augustino, ameonyesha tuzo hiyo mbele ya wafanyakazi wenzake, amesisitiza kuwa ushindi huo ni matokeo ya kazi ya pamoja, nidhamu na kuwapa kipaumbele wateja katika kila hatua ya utoaji huduma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mikakati na Data wa Benki ya Absa Tanzania, John Mosha, akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, amesema: tuzo hiyo inaonyesha wazi kuwa mikakati ya benki hiyo ya kuimarisha huduma, kuwekeza kwenye mifumo ya kidijitali na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wateja imeonekana na kuthaminiwa na walaji.
“Ushindi huu ni uthibitisho kwamba tuko karibu na wateja wetu na tunasikiliza mahitaji yao. Tutaendelea kuboresha huduma, kuongeza ubunifu na kuhakikisha kila mteja anafikiwa kwa wakati na kwa njia rahisi,” amesema Mosha.

Tuzo za Chaguo la Walaji hutolewa kila mwaka kwa taasisi na makampuni mbalimbali ambayo yamepigiwa kura na watumiaji wa bidhaa na huduma, zikilenga kutambua na kuthamini ubora, ubunifu, huduma bora kwa mteja na mchango katika jamii.
Kupatwa kwa tuzo hii kunaiweka Absa katika nafasi ya juu zaidi miongoni mwa taasisi za kifedha zinazotegemewa na kupendekezwa na wateja katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi