Na Queen Lema,Timesmajiraonline,Arusha
KAMPUNI ya Usafiri wa Mtandaoni(BOLT)imesema kampuni hiyo imekuwa sehemu muhimu ya mabadiliko ya kiuchumi nchini kutokana na kuwafungulia vijana wengi milango ya ajira kupitia usafirishaji.
Hayo yamesemwa na Meneja mahusiano ya umma kutoka Kampuni ya kimataifa ya usafiri bolt Tanzania,Gilbert Ginono wakati akitoa mada katika Mkutano wa wataalamu wa mawasiliano zaidi ya 100 kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika jijini Arusha.
Ginono amesema kuwa Bolt imekuwa mkombozi kwa vijana wengi kupata ajira na kupata fursa ya kujipatia kipato kwa usafirishaji kwa njia ya mtandaoni.
“Vijana wengi sasa wanategemea Bolt kupata kipato cha kila siku na kwamba mfumo huo wa kidigitali umeongeza mzunguko wa fedha na kutoa matumaini kwa wanaotafuta ajira mijini lakini pia umerahisisha wananchi kupata huduma za usafiri wa haraka na salama,”amesema Ginono.
Aidha Ginono amesema kuwa Bolt imekuwa msaada pia kwa wanawake wanaotaka kutoa huduma za ambapo amesema hadi sasa wanawake wameongezeka kwa kasi katika utoaji wa huduma hiyo.
Ameeleza kuwa uwepo wa wanawake kwenye mfumo wa Bolt umeongeza usawa wa kiuchumi na kutoa nafasi kwa familia nyingi kuinuka kimaendeleo.
Aidha amesema huduma ya Bolt imeongeza ushindani katika sekta ya usafiri wa mijini na kuleta ubora wa huduma pamoja na fursa mpya za kifedha kwa madereva katika mikoa mbalimbali ya nchi huku akisisitiza kuwa Bolt haijaja kutoa huduma pekee bali imekuja kujenga ajira endelevu na kuchangia pato la taifa kupitia teknolojia.
Mkutano huo unaojulikana kama East Africa PR Week umehusisha maofisa uhusiano kutoka sekta mbalimbali huku kampuni ya usafiri wa mtandaoni Bolt ikivuta hisia za wengi kutokana na mchango wake katika kuleta ajira na kuchochea uchumi wa Tanzania.
Kwa upande wake Mwanzilishi wa Chama cha Maofisa Uhusiano Tanzania Loti Makuza alisema mkutano huo umelenga kuongeza uelewa kwa maofisa uhusiano ili wawe tayari kuijenga imani kati ya serikali na wananchi.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi