
Na WMJJWM – Dodoma
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amefungua kikao cha viongozi na waratibu wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi nchini kwa njia ya mtandao, kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha majukwaa hayo katika ngazi zote nchini.
Katika hotuba yake, Dkt. Gwajima ametoa rai kwa viongozi kuendelea kudumisha ustawi wa wanawake kupitia kuhamasisha umoja, uanzishwaji wa vikundi, na kuimarisha sauti ya pamoja ya wanawake katika maendeleo ya taifa.
“Majukwaa haya yameanzishwa kutoa fursa kwa wanawake kukutana, kujengeana uwezo kiuchumi, na kuhakikisha sauti yetu inasikika katika maendeleo ya taifa,” amesema Dkt. Gwajima.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa majukwaa kuendelea kufuata malengo ya kuanzishwa kwake, ikiwemo kujenga uwezo wa wanawake kiuchumi, kukuza uzalendo, na kutokomeza ukatili. Amesema pia Wizara itafanya ufuatiliaji wa kina kuanzia ngazi ya vijiji ili kubaini maendeleo na changamoto halisi za vikundi kwa kwenda na utaratibu wa kasi Zaidi, Karibu Zaidi na Wananchi maarufu kwa kifupi (KAZAKAZAWA) – .
Dkt. Gwajima ametaka majukwaa kuimarisha mshikamano, kuongeza wanachama, na kuhakikisha wanawake wanatumia majukwaa hayo kujenga nguvu ya pamoja katika uchumi, uzalendo, na kupambana na ukatili. Amesisitiza kuwa taarifa sahihi za vikundi, pamoja na mfumo mzuri wa kupokea kero na mrejesho, vitasaidia kuongeza ufanisi na kasi ya kuwafikia wanawake nchini.
Akihitimisha, Waziri Gwajima amewashukuru viongozi wa majukwaa kwa uaminifu na kujitoa, akiwataka washirikiane kuandaa mapendekezo ya utekelezaji wa mpango aliouwasilisha. Amewahakikishia kuwa Serikali inathamini nafasi yao katika kufanikisha maono ya Rais Samia ya kuwawezesha wanawake kiuchumi na kijamii.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa, Naibu Waziri Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb) ameushukuru uongozi wa wizara na Rais Samia kwa kumwamini, akieleza kuwa bado anaendelea kujifunza taratibu, majukumu, na mfumo wa kazi wa wizara hiyo. Amewaomba viongozi wa majukwaa na watendaji kumpa ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kuongeza nguvu katika kuharakisha maendeleo ya wanawake nchini.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. John Jingu, amesisitiza umuhimu wa ushikamano kati ya wizara, TAMISEMI, na majukwaa katika ukusanyaji na matumizi sahihi ya takwimu. Amesema mfumo unaojengwa utarahisisha check and balance, kuongeza uwazi, na kutoa taarifa za uhakika zitakazowezesha maamuzi ya haraka na yenye tija. Ametoa wito kwa waratibu wa mikoa na wilaya kuhakikisha taarifa zote za vikundi zimekamilika ili Wizara iweze kuanza utekelezaji wa kazi kwa kasi na weledi.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina