Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuimarisha malezi na makuzi chanya ya watoto nchini.
Akizungumza na vikundi vya malezi na matunzo ya watoto katika kata ya v Ihumwa, mkoani Dodoma, Mhandisi Mahundi alisema Serikali inatambua umuhimu wa vikundi vya maendeleo kama chachu ya uwezeshaji kiuchumi, lakini akaeleza kuwa vikundi hivyo vinapaswa pia kutumika kama majukwaa ya kuelimishana na kukumbushana majukumu ya msingi katika malezi ya watoto.
“Nimekuja hapa na wenzangu kushirikishana fursa za kiuchumi kupitia vikundi vyenu, lakini pia kuvitumia vikundi hivi kama jukwaa la kukumbushana wajibu wetu wa malezi chanya ya watoto na familia,” alisema.
Naibu Waziri alifafanua kuwa familia, ambayo inaundwa na baba, mama na watoto, ni taasisi muhimu na msingi wa jamii yoyote duniani. Akasisitiza kuwa familia ina jukumu kubwa la kutoa huduma za msingi, kusimamia malezi na makuzi bora ya watoto, pamoja na kurithisha mila na tamaduni nzuri kwa vizazi vijavyo.
Aidha, aliwakumbusha wazazi wote kujitathmini kuhusu utekelezaji wa majukumu yao ya kifamilia. Alieleza kuwa changamoto nyingi za maadili na tabia kwa watoto zinachangiwa na wazazi au walezi kutokutimiza wajibu wao ipasavyo.
“Ni ukweli usiopingika kwamba wazazi au walezi tulio wengi hatutimizi wajibu wetu hasa katika malezi na makuzi ya watoto,” alisema huku akisisitiza kuwa msingi wa malezi bora huanza tangu mtoto akiwa tumboni.
Mhandisi Mahundi aliainisha majukumu makubwa matatu ambayo kila mzazi au mlezi anatakiwa kuyazingatia kuwa ni pamoja na kumpatia mtoto mahitaji ya msingi ikiwemo chakula, afya, elimu na malazi salama.
Mengine ni kumlinda mtoto dhidi ya ukatili wa aina zote, hususan unyanyasaji wa kijinsia unaowakumba watoto wengi bila wazazi kutambua mapema na kujenga utamaduni wa kuzungumza na mtoto mara kwa mara, ili kujua maendeleo yake na changamoto anazokabiliana nazo, pamoja na kukuza ukaribu kati ya mzazi na mtoto.
Alisema kuwa ukosefu wa mawasiliano kati ya mzazi na mtoto umekuwa chanzo cha watoto wengi kuficha madhila, ikiwemo matukio ya udhalilishaji kama ubakaji mpaka madhara yanapokuwa makubwa.
Akigusia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, Naibu Waziri alisema kuwa pamoja na manufaa makubwa yanayoletwa na mitandao ya kijamii, bado kumekuwa na changamoto kubwa za mmomonyoko wa maadili kwa watoto.
“Ni zama zao, hatuwezi kuwakataza kutumia mitandao, lakini wajibu wetu kama wazazi na walezi ni kuwa karibu nao na kuwaongoza,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa utandawazi umewafanya watoto kuwa wepesi kuiga tamaduni za nje, hivyo wazazi wanapaswa kuongeza uangalizi na malezi kuanzia umri wa awali.
Katika hotuba yake, Naibu Waziri aliweka bayana ongezeko la ukatili wa mtandaoni unaowalenga watoto, akisema kuwa takwimu zinaonyesha watoto 67 kati ya 100 wenye umri wa miaka 12–17 wanatumia vifaa vya mawasiliano vyenye intaneti ambapo miongoni mwao, watoto 4 kati ya 100 tayari wameshawahi kufanyiwa ukatili wa aina fulani mtandaoni.
Ametaja baadhi ya matukio hayo kuwa ni pamoja na kurubuniwa kushiriki vitendo vya kingono, kutishiwa, kuombwa kutuma picha na video zisizofaa na kusambaziwa maudhui yao bila ridhaa.
Alisisitiza kuwa wazazi wanapaswa kufuatilia matumizi ya mitandao kwa watoto, kuwalinda na kuwafundisha namna ya kutumia teknolojia kwa usalama.
Aidha, Mhandisi Mahundi aliwataka wanakikundi, wazazi na walezi kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wanapata mazingira salama, yenye upendo, uongozi na malezi bora ili waweze kukua na kuwa nguzo imara ya familia na Taifa.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina