Na Mwandishi wetu,Timesmajira
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amezindua onesho maalum la Historia ya Reli ya Tanzania–Zambia (TAZARA) linaloendelea katika Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam, likilenga kutoa fursa kwa Watanzania kujifunza historia ya reli hiyo na mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi
Onesho hilo linajumuisha michoro, machapisho na vielelezo mbalimbali vya kihistoria na limehudhuriwa na mabalozi, viongozi wa serikali, wananchi pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga. Litaendelea kwa kipindi cha miezi miwili.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Novemba 26,2025 na kuandaliwa na ubalozi wa Jamhuri ya watu wa china kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa Dkt. Kijaji alisema onesho hilo ni “darasa hai” litakalotoa elimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo kuhusu uongozi wa maono wa waasisi wa Taifa katika kuimarisha uhuru wa kiuchumi na ushirikiano wa kimataifa.

“TAZARA ni alama muhimu ya mshikamano kati ya Afrika na China. Imeendelea kuwa miongoni mwa miundombinu yenye mafanikio makubwa katika kusafirisha watu na bidhaa kati ya Tanzania, Zambia na China,” amesema Dkt. Kijaji.

Ameongeza kuwa reli hiyo, iliyojengwa mwaka 1970 kwa ushirikiano na Serikali ya China, ni urithi muhimu ulioachwa na waasisi wa Taifa na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuuthamini na kuuendeleza chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha,ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea onesho hilo ili kuenzi urithi wa Taifa na kuimarisha misingi ya amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema TAZARA imechangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya Tanzania na Zambia, pamoja na kusaidia harakati za kupinga ukoloni na ukandamizaji Kusini mwa Afrika.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako