March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndejembi aitaka PURA kuweka mikakati itakayoongeza kasi utafutaji wa mafuta, gesi asilia

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online-Dar

WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi ameitaka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuja na mikakati thabiti itakayosaidia kuongeza kasi ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Ndejembi ameyasema hayo Novemba 24, 2025 Jijini Dar-es-Salaam katika kikao chake na uongozi wa PURA.

Katika kikao hicho, Ndejembi amesema kuwa, anatarajia kuona PURA inaweka nguvu katika kuandaa na kutekeleza mikakati itakayoongeza kasi ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini kwa kuwa tafiti hizo zinachukua muda mrefu.

“Ninatarajia kuona PURA inaandaa na kutekeleza mikakati itakayochagiza utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu mbalimbali vikiwemo Ruvu, Mkuranga na Tanga, mikakati itakayoeleza bayana nini kifanyike ili tuweze kupata matokeo tarajiwa,”amesema.

Sambamba na hilio, Ndejembi ameitaka PURA kuendelea kutoa ushauri wenye tija kwa Wizara kuhusu namna ya kufanya mazingira ya uwekezaji katika mkondo wa juu wa petroli kuwa shindani,ili nchi inapokwenda kwenye duru ya tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia (5th licencing round) matokeo tarajiwa yapatikane.

“Kabla ya kwenda kwenye duru ya tano ya kunadi vitalu natarajia kuona PURA inatushauri Wizara kuhusu nini hatua za kufuata ili tufanye mazingira yawe rafiki kwa wawekezaji tunaowatarajia huku tukilinda maslahi ya nchi yetu. Nanatarajia ushauri huo uje haraka ili tuweze kuufanikisha” alisistiza Ndejembi.

Ndjejembi pia ameweka bayana kuwa kufanikisha duru ya tano ya kunadi vitalu si tu kutaongeza mapato kwa Serikali lakini kama Wizara itakuwa imeiwezesha Serikali kuacha alama chanya katika sekta.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni kwa niaba ya menejimenti ya PURA amemshukuru Waziri Ndejembi na uongozi mzima wa Wizara kwa kutenga muda wao kufanya kikao na menejimenti ya PURA.

Sangweni ameahidi kuwa, PURA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kufikia malengo ya kisekta na kuchangia katika Dira 2050.