Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Imeelezwa kuwa Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania,inaendelea kuimarisha usalama wa mabwawa nchini,ambayo ni muhimu katika ustawi jamii,uchumi na uendelevu wa mazingira,pia ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yamebainishwa Novemba 21,2025 na Kaimu Mkurugenzi Rasilimali za Maji Wizara ya Maji,Robert Sunday,wakati akufunga kongamano la mwaka 2025 la Usalama wa Mabwawa kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo ,Jumaa Aweso,lililofanyika mkoani Mwanza kwa siku tatu likiwa na kaulimbiu isemayo “Maandalizi ya Dharura na Mwitikio wa Tailing na Mabwawa ya Maji”.

Ambapo amesema, Wizara ya Maji, kupitia Kurugenzi ya Rasilimali za Maji, ina jukumu la kusimamia na kufuatilia uzingatiaji wa usalama wa mabwawa yote mawili ya maji na tope sumu kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Sura. 331 na Kanuni zake za Usalama wa Mabwawa.
“Wizara inahakikisha kwamba miundombinu hii muhimu inaendelezwa, inaendeshwa na kutunzwa kwa namna ambayo inalinda watu, mali na mazingira,”amesema.
Sunday amesema,mabwawa yamekuwa na jukumu muhimu kama vifaa vya kuhifadhi maji kusaidia ustawi wa kijamii, maendeleo ya kiuchumi na uendelevu wa mazingira.
“Mabwawa ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa maji unaotoa mazingira wezeshi kwa umwagiliaji na usalama wa chakula,uzalishaji wa umeme wa maji na usalama wa nishati, kudhibiti mafuriko, kudhibiti ukame na kutoa maji ya uhakika kwa matumizi ya nyumbani, viwandani na kisekta,”amesema Sunday.
Amesema maeneo mbalimbali nchini hupitia vipindi vya mvua nyingi vinavyosababisha mafuriko na vipindi vya ukame vinavyopunguza upatikanaji wa maji,hivyo Wizara kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania,utaendelea kuimarisha mabwawa hayo ili yasiweze kuleta athari.
“Mabwawa ya maji ya kawaida na ya tope sumu ni miundombinu muhimu ambayo lazima ihifadhiwe na kusimamiwa kwa umakini ili yasigeuke kuwa chanzo cha majanga kwa maisha ya watu, mali na mazingira,”amesema Sunday.
Sanjari na hayo amesema, usimamizi bora wa usalama wa mabwawa ni muhimu ili kulinda maisha, kulinda mifumo ikolojia na kuhakikisha uendelevu wa manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake, Mhandisi kutoka Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO)
Michael Laurent, pia ni mtaalamu ambaye amethibitishwa na Wizara ya Maji kusimamia mabwawa ya maji,alisema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha maeneo ya chini ya mabwawa yanayosimamiwa na shirika hilo yanabaki salama endapo kutatokea mafuriko, na kwamba wahandisi wao wamepewa mafunzo ya kuzuia madhara yoyote yanayoweza kutokea.

Mhandisi Happines Kihedu, kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji,amesema tume hiyo hujenga mabwawa ya umwagiliaji ili kuwasaidia wakulima kuzalisha zaidi ya msimu mmoja na kuongeza usalama wa chakula.
Hivyo kupitia kongamano hilo,wamejifunza zaidi kuhusu usalama wa mabwawa na namna wanavyopaswa kuzingatia sheria na taratibu zote ili kulinda wakulima na wananchi wanaoishi karibu na mabwawa.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi