Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Amiri Mkalipa,ameagiza zoezi la upandaji miche ya matunda wilayani humo kuwa endelevu pamoja na utoaji wa elimu ya lishe kwa vitendo(shamba darasa) ili kuwa na watoto wenye afya bora.
Mkalipa amezungumza hayo Novemba 20,2025 katika maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa,ambayo kwa Wilaya ya Ilemela yalifanyika mtaa wa Imalang’ombe Kata ya Sangabuye.

Ambapo amesema dhumuni la maadhimisho hayo kni kuongeza uelewa katika jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa jamii.
“Napenda kusisitiza upandaji wa miche ya matunda uwe endelevu sambamba na utoaji elimu ya lishe kwa vitendo.Pelekeni huduma hii shuleni na kwenye zahanati nyingi zaidi ili watoto wetu na jamii kwa ujumla waendelee kujifunza juu ya lishe kwa vitendo,”amesema Mkalipa.
Pia amewaagiza wataalamu wa lishe wilayani Ilemela kuweka mkazo kwenye utoaji elimu ya lishe katika maeneo yote ya Wilaya hiyo,kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kuondokana na maradhi yatokanayo na ukosefu wa lishe bora na kuwa na watoto wenye afya.
Sanjari na hayo Mkalipa ametoa wito kwa kina baba kutimiza wajibu wao katika malezi ya watoto kwani kuna maradhi kama vile udumavu na utapiamlo wakati mwingine husababishwa na wazazi kutokutimiza wajibu wao.

Kwa upande Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Ummy Wayayu, amesema elimu ya masuala mbalimbali ya lishe na afya iliyotolewa katika maadhimisho hayo anaamini kuwa jamii itakwenda kuyafanyia kazi kikamilifu pamoja na kuwa mtazamo chanya.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli na afua za lishe Halmashauri ya Manispaa Ilemela,Ofisa Lishe qa Halmashauri hiyo,Pili Kasim,amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kupungua kwa hali ya utapiamlo kutoka asilimia 2.9 hadi asilimia 2.0.
Pia Halmashauri hiyo imefanikiwa kuanzisha kilimo cha mazao kwenye shule za msingi na sekondari 22, bustani 17 za mbogamboga pamoja na vituo vitatu vinavyotoa huduma za afya lengo ikiwa ni kuwasaidia wanafunzi na jamii kujifunza kwa vitendo elimu ya lishe.
“Nitoe wito kwa jamii kuhakikisha inafuata mtindo bora wa maisha pamoja na kuzingatia ulaji unaofaa ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza,”amesema Pili.
Naye mtaa wa Imalang’ombe Jeremia Daniel,amewaasa wazazi na walezi kuwahudumia watoto wao na kuwapatia huduma ya lishe bora ili wakue katika hali nzuri.
Huku Semeni Peter,ametoa wito kwa kina baba na kina mama kushiriki kikamilifu katika matukio kama hayo.

Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo,”Afya ni mtaji wako;Zinagtia unachokula” yameenda sambamba na huduma za utoaji wa matone ya vitamin A na dawa za minyoo kwa watoto chini ya umri wa miaka 5, upimaji wa HIV, homa ya ini, saratani ya matiti, huduma za macho, masikio na kinywa pamoja na shughuli mbalimbali za utoaji wa elimu ya lishe.
Pia ulaji unaofaa kwa mama mjamzito na mama anayenyonyesha, umuhimu wa kutumia vyakula vilivyoongezwa virutubisho, jiko darasa, ugawaji wa unga wa lishe sambamba na upandaji wa miti ya matunda.



More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina