March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Airtel Africa, Nokia washirikiana kujenga mkongo wa mawasiliano Afrika

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

AIRTEL Africa, mmoja wa watoa huduma wakubwa wa mawasiliano na huduma za fedha kwa njia ya simu katika nchi 14 za Afrika, imeshirikiana na Nokia kujenga mtandao wa kisasa wa mkongo wa mawasiliano wa ardhini (terrestrial fiber).

Mkongo huo wenye uwezo mkubwa unaounganisha nchi za Afrika Mashariki na Kati kupitia huduma yake ya hali ya juu ya fiber, Airtel Africa Telesonic.

Mradi huo wa kimkakati unalenga kuunganisha mataifa mbalimbali ya Afrika na kuzikutanisha na mkongo wa mawasiliano unaopita baharini na mifumo ya ardhini, hatua itakayoboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma bora za intaneti barani Afrika.

Hatua hiyo inatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya jamii kwa kutoa huduma ya miundombinu ya kidijitali yenye ubora, uhakika na gharama nafuu.

Aidha, Mradi huo ambao ulitangazwa katika Mkutano wa 28 wa AfricaCom, wenye mkusanyiko mkubwa zaidi duniani wa viongozi wa sekta ya mawasiliano wanaolenga kutoa huduma katika nchi za Afrika.

Mradi huo pia, utawezesha mkongo wa mawasiliano wa ardhini na baharini waza 2Africa kuunganishwa moja kwa moja na mitandao ya ardhini, hivyo kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu na kwa kasi ya juu.

Kupitia matumizi ya miundombinu ya fiber ya Telesonic pamoja na mifumo ya mkongo wa mawasiliano wa ardhini za baharini, mradi huo utatoa suluhisho la kushughulikia ongezeko la mahitaji ya data ya jumla (wholesale data) barani Afrika na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa kutumia teknolojia ya Nokia 1830 Photonic Service Switch (PSS), mtandao huo mpya utaweza kubeba hadi Terabiti 38 kwa sekunde (38 Tbps), hivyo kuwezesha usafirishaji wa data kwa kasi ya juu zaidi.

Mtandao wa DWDM unaojengwa, wenye jumla ya nodi 139 na kuunganisha nchi kadhaa, unaongozwa na injini ya mifumo ya kisasa ya Nokia ya Photonic Service Engine (PSE), ambayo ni ya kasi ya juu na yenye ubora wa kipekee.

Zaidi ya kujenga miundombinu ya kidijitali barani Afrika, mradi huo pia unaonesha dhamira ya Telesonic katika kuwawezesha wafanyabiashara, sekta ya elimu na huduma za afya kupata huduma bora za kidijitali.

Akizungunzia hilo, Afisa Mkuu wa Tecknolojia wa Airtel Afrika, Razvan Ungureanu amesema utekelezaji wa jukwaa la Nokia 1830 Photonic Service Switch, ni hatua muhimu sana katika kuboresha miundombinu ya mtandao barani Afrika.

“Teknolojia hii itatuwezesha kuongeza uwezo wa mtandao na kutoa huduma za kasi ya juu zaidi ili kukidhi mahitaji makubwa ya matumizi ya intaneti.

“Kwa kutumia Photonic Service Engine ya Nokia katika mtandao wetu wa DWDM unaovuka nchi mbalimbali, tunafungua njia kwa maendeleo makubwa na fursa mpya barani Afrika,” amesema Razvan.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Afrika Telesonic, PD Sarma alisema ushirikiano wao na Nokia ni hatua muhimu katika kuimarisha miundombinu ya kidijitali barani Afrika.

“Kupitia miundombinu hii ya suluhisho za kisasa za fiber kutoka Nokia, tunalenga kukidhi mahitaji ya data yanayoongezeka ya data katika kila wakati barani hili.

“Mtandao huu utaendesha ukuaji wa uchumi, kuwawezesha wananchi, na kufungua fursa mpya kwa biashara na watu binafsi,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Kundi la Ukuaji la Miundombinu ya Mitandao ya Nokia kwa Mashariki ya Kati na Afrika, Samer Lutfi amesema wanajivunia kushirikiana na Airtel Africa Telesonic, katika mradi huo mkubwa wa kuboresha upatikanaji wa huduma za intaneti barani Afrika.

“Teknolojia yetu ya DWDM yenye uwezo mkubwa na uthabiti wa hali ya juu imeundwa kusaidia taasisi na biashara kusukuma mbele mageuzi ya kidijitali na kukuza uchumi wa eneo hili.

“Mradi huu unadhihirisha ni ushahidi wa dhamira yetu ya pamoja ya kuunganisha jamii na kuhimiza maendeleo,”amesema.