March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Othman :Wazanzibar lazima wapate haki yao ya Serikali walioichagua

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema kuwa ni lazima Wazanzibari wapate haki yao ya serikali walioichagua kwa misingi ya kidemokrasia.

Akizungumza katika Afisi ya chama hicho Mtambile, Wilaya ya Mkoani, Othman alisema chama chake hakitokuwa tayari kushiriki mazungumzo yoyote yanayolenga kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) bila ya kuheshimu misingi ya haki na matokeo halisi ya uchaguzi uliopita.

“Wanafanya wanayofanya kwa sababu wanaamini stahiki yetu ni nafasi ya Makamu wa Kwanza tu, jambo hili lazima likome,”amesema Othman.

Amefafanua kuwa mnamo Novemba 4, Katibu Mkuu Kiongozi aliwaandikia barua ya kuomba jina la Makamu wa Kwanza wa Rais kutoka ACT Wazalendo, lakini chama hicho hakikupeleka jina hilo kwa kuwa halikuridhika na mazingira ya kisiasa yaliyopo.

Othman ameongeza kuwa uchaguzi uliopita uligubikwa na hila nyingi zilizoharibu misingi ya haki na uhuru, hivyo mazungumzo yoyote yatakayofanyika ni lazima yaendane na maamuzi ya wananchi yaliyodhihirika kupitia uchaguzi huo.

Mapema Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ismail Jussa, amesema chama chao hakitakuwa tayari kuingia katika mazungumzo yoyote na Chama cha Mapinduzi (CCM) ikiwa lengo ni kufunika ukweli au kupitisha mambo kwa urahisi.

Jussa amesema kuwa mazungumzo yoyote kati ya vyama hivyo lazima yajikite katika kuhakikisha haki inatendeka, na kwamba wale wote waliohusika kuvuruga uchaguzi uliopita wanapaswa kuwajibishwa mara moja.

Amesisitiza kuwa ACT-Wazalendo haitakubali maelewano ya “kuku lala” yanayolenga kupoteza ukweli na kuendeleza ukandamizaji wa demokrasia visiwani Zanzibar.