March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‎Mbunge Ndoinyo aahidi kuibadilisha Ngorongoro kuwa kitovu cha maendeleo

‎Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

‎Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Mheshimiwa Yanick Ndoinyo, amesema amejipanga kuibadilisha na kuijenga upya Wilaya ya Ngorongoro kwa kugeuza changamoto zilizopo kuwa fursa za maendeleo kwa wananchi wa eneo hilo.

Akizungumza hivi karibuni mara baada ya kuapishwa kuwa Mbunge wa Bunge la 13, Ndoinyo alisema wananchi wa Ngorongoro wamemkabidhi dhamana hiyo kwa matumaini makubwa, huku akiahidi kutumia nafasi hiyo kuleta mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni wilayani humo.

Ngorongoro ni jimbo la kimkakati kwa sababu ni eneo maarufu kwa utalii, ufugaji na kilimo. Nafahamu nina majukumu mazito, lakini nimejipanga kuhakikisha changamoto zilizopo zinageuzwa kuwa fursa za maendeleo,” alisema Ndoinyo.

‎Amesema moja ya vipaumbele vyake ni kuboresha miundombinu ya barabara, hasa kujenga barabara ya lami itakayounganisha wilaya hiyo na mkoa wa Arusha ili kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa.

‎ “Ukienda makao makuu ya wilaya, utafikiri bado upo kijijini. Tunataka tubadilishe sura ya Ngorongoro iwe na hadhi yake. Kupitia barabara ya lami, tutafungua uchumi na kuongeza kasi ya maendeleo,” alifafanua.

‎Mbunge huyo pia amesema anataka kuona sekta ya utalii inaimarika kwa kutumia fursa zilizopo kwa asilimia 100 badala ya 50 kama ilivyo sasa, ili Ngorongoro iwe kivutio kikubwa cha utalii nchini na duniani.

‎Vilevile, ameweka mkakati wa kubadilisha mfumo wa ufugaji kutoka wa kimila hadi wa kibiashara ili wafugaji waweze kunufaika zaidi na rasilimali zao.

‎ “Tunataka sekta ya ufugaji iwe ya kibiashara. Hii itasaidia kuongeza kipato cha wananchi na mapato ya wilaya,” alisema.

‎Ndoinyo pia alibainisha mpango wa kuanzisha mfuko wa mitaji utakaowezesha wananchi kupata mikopo na mitaji ya kuanzisha biashara ndogo na za kati, jambo litakaloinua kipato cha kaya.

‎Ameeleza kuwa utekelezaji wa mipango hiyo unahitaji ushirikiano kati ya serikali na wananchi, akisisitiza kuwa mahusiano mazuri kati ya pande hizo mbili ndiyo msingi wa mafanikio.

‎“Lengo langu ni kuhakikisha serikali, wilaya, wananchi na taifa wanazungumza lugha moja kuhusu maendeleo. Huo ndio msingi wa mafanikio yetu,” alisema Mbunge huyo.

‎Aidha, aliwataka Watanzania kuwa na imani na Bunge la 13, akisema lina dhamira ya dhati ya kushughulikia matatizo ya wananchi kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Watanzania waendelee kuwa na imani na Bunge hili kwa sababu lina wabunge wengi wa CCM ambao wanafahamu changamoto za wananchi na namna ya kuzitatua,” alisema.

‎Ndoinyo alihitimisha kwa kusema kuwa katika awamu yake ya kwanza, atatumia uhusiano wake wa kimataifa kuvutia miradi ya maendeleo na kuboresha taswira ya Bunge kwa wananchi wa Ngorongoro.