Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Arusha, Chiku Athumani, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mafanikio makubwa aliyoyapata katika kipindi chake cha uongozi, hususan katika sekta ya afya, huku akiahidi kuweka nguvu zaidi katika kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto nchini.
Akizungumza katika viwanja vya bunge na waandishi wa habari mara baada ya kuapishwa jijini Dodoma, Chiku alisema ushindi wa kishindo wa asilimia 97 alioupata Rais Samia ni ishara tosha ya imani kubwa ambayo Watanzania wanayo kwa uongozi wake wenye tija na matokeo chanya.
“Kama mwakilishi mwanamke kutoka Mkoa wa Arusha, ninasimama kifua mbele kumpongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa aliyoyafanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake, hasa katika eneo la afya ya mama na mtoto,” alisema Chiku.
Ameeleza kuwa hatua za Rais Samia zimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua na watoto wachanga nchini.
“Kabla hajaingia madarakani, katika kila vizazi 100,000, wanawake 556 walikuwa wanapoteza maisha wakati wa kujifungua, lakini sasa idadi hiyo imepungua hadi kufikia vifo 104 pekee. Huu ni ushahidi wa mafanikio makubwa katika sekta ya afya,” aliongeza.
Chiku alisisitiza kuwa kama mama na mwakilishi wa wanawake, ataendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha afya ya mama na mtoto inakuwa kipaumbele cha kwanza katika utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge.
Aidha, alitoa pongezi kwa Rais Samia kwa jitihada za kuboresha sekta ya elimu nchini, akibainisha kuwa watoto sasa hawatembei umbali mrefu kama zamani kufika shule, ambapo kwa sasa wastani wa umbali huo umepungua hadi kilometa mbili pekee Kutoka umbali wa hadi kilomita Tano na zaidi.
“Kazi kubwa ya Bunge ni kuisaidia na kuishauri serikali. Sisi ni watunga sheria, hivyo tunapaswa kuhakikisha kwamba yale tunayoyapitisha bungeni yanasimamiwa kwa umakini na uthubutu mkubwa ili wananchi wanufaike moja kwa moja,” alisema Chiku.
Chiku ameahidi kutumia nafasi yake bungeni kuendelea kupigania masuala ya afya, elimu na uwezeshaji wa wanawake, akisema ni maeneo muhimu katika kuleta maendeleo endelevu kwa Taifa.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina