Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Rukwa
NAIBU Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba amewahakikishai wakulima wa mahindi mkoani Rukwa kuwa mradi wa ujenzi wa vihenge vya kisasa vya kuhifadhia mazao, utakapokamilika utatatua tatizo la soko kwa wakulima.
Akizungumza mkoani hapa mwishoni mwa wikili, Mgumba amesema mradi huo utakapokamilika utaondoa tatizo kwa wakulima ambao kwa msimu wa 2019/20 wamekuwa wakipata tabu kutokana na wanunuzi wengi kutoka nchi za jirani, kufunga mipaka yao kutokana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19) na hivyo kushindwa kuingia nchini na kununua mazao hayo.
Mgumba amesema, hivi sasa NFRA, wamesimama kununua mazao kwa sababu ya kufanya tathmini kwa wakulima wanaoidai fedha ambapo hadi kufikia mwishoni mwa wiki, hakukuwa na mkulima hata mmoja anayedai fedha hizo.
Ameongeza kuwa, kutokana na maghala mengi ya NFRA kujaa, imewawasababishia kushindwa kununua mengine huku akielezea kuwa serikali haitaki kuwakopa wakulima, wakitambua kuwa wakulima hao hivi sasa wanajiandaa na msimu mpya wa kilimo.
“Lakini la pili ambalo walisimama na sehemu nyingine wakaendelea kusimama ni kutokana na maghala yamejaa, pakuweka hakuna, ushahidi ni nyinyi watu wa Laela ndiyo maana nikataka kuhakikisha kwa kuingia ndani kwanza, nimekuta humo ndani kumejaa,” amesema.
Wakati akitoa taarifa ya ununuzi wa mahindi pamoja na uhifadhi wake katika Mikoa ya Rukwa na Katavi, Kaimu Meneja wa Kanda ya Sumbawanga inayojumuisha mikoa hiyo, Marwa Range amesema kwa sasa NFRA wanaweza kuhifadhi mazao kwa jumla ya tani 38,500.
Amesema, na mradi wa maghala na vihenge utakapokamilika uwezo wa kuhifadhi mazao utaongezeka hadi kufikia tani 58,500 kwa Mkoa wa Rukwa pekee, huku Mkoa wa Katavi ukiwa na uwezo wa kuhifadhi tani 500 kwa sasa, lakini mradi huo ukikamilika mkoa utaweza kuhifadhi tani 28,000 na kuifanya NFRA Kanda ya Sumbawanga kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 86,500 za mazao.
Kwa upande wake Mhandisi Mkaazi wa mradi wa ujenzi wa vihenge kutoka Wakala wa Majengo (TBA) mkoani Rukwa, Mhandisi Haruna Kalunga amesema, mradi huo unaotarajiwa kukamilika Machi 3 mwakani utafikia asilimia 60 mwishoni mwa mwezi huu na kubakisha asilimia 40, inayotarajiwa kumaliza ndani ya miezi iliyobakia.
Katika hatua nyingine, Mgumba amewasifu wakandarasi wa ujenzi wa vihenge hivyo vya kisasa kwa kuwa ndani ya wakati pamoja na shughuli zao hizo kuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo janga la Corona, lakini wameweza kufanikisha kuifanya kazi hiyo kwa wakati na kuwatumia wafanyakazi Watanzania kwa asilimia kubwa na hivyo kuinufaisha nchi kwa kuzalisha wataalamu wa ujenzi wa vihenge hivyo.
%%%%%%%%%%%
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia