Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
JAMII imeshauriwa kuwa na utaratibu wa kufanya uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti mara kwa mara ili kutambua visababishi na dalili za mwanzo za ugonjwa huo, hatua ambayo inaweza kusaidia kuokoa maisha ya wanawake wengi nchini.
Ushauri huo umetolewa jijini Dar es Salaam leo Oktoba 24, 2025, katika mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wanahabari wanawake kuhusu uchunguzi wa mapema na kinga dhidi ya saratani ya matiti, yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA).
Akizungumza katika mafunzo hayo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani kutoka Hospitali ya Ocean Road, Dkt. Faraja Kiwanga, amesema ni muhimu kila mtu kufanya uchunguzi mara kwa mara kwani ugonjwa wa saratani unaweza kumkumba mtu wa jinsia na umri wowote.
“Saratani inazuilika na inatibika. Hata hivyo, bado tunakabiliwa na changamoto ya utoaji elimu kwa jamii ili wajue visababishi na jinsi ya kujiepusha navyo, ikiwemo kubadili mtindo wa maisha usiofaa,” amesema Dkt. Kiwanga.
Dkt. Kiwanga amewleza kuwa takwimu zinaonyesha asilimia 31 ya wagonjwa wa saratani ya matiti hufika hospitalini katika hatua za awali, huku asilimia 75 wakichelewa kufika, jambo linalopunguza mafanikio ya matibabu.

Ametaja dalili za awali za saratani ya matiti kuwa ni uvimbe au donge kwenye titi, kubadilika kwa umbo au ngozi ya titi, kutoka kwa majimaji yasiyo ya kawaida kwenye chuchu, maumivu, au uvimbe kwenye kwapa au shingo.

Aidha, amesema matibabu ya saratani hutegemea hatua ya ugonjwa na yanaweza kujumuisha upasuaji, tiba ya mionzi (radiotherapy), tiba ya kemikali (chemotherapy), tiba ya homoni, au immunotherapy.
Dkt. Kiwanga pia amehimiza jamii kubadili mifumo ya maisha kwa kufanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki, kuepuka vyakula vyenye mafuta mengi na nyama nyekundu, pamoja na kuacha uvutaji sigara na unywaji pombe.
“Ni muhimu pia kufanya uchunguzi wa kitabibu mara kwa mara katika vituo vya afya vilivyo karibu,” amesisitiza

Awali, akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, Meneja wa Mpango Mkakati wa chama hicho, Sylivia Daulinge, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya maadhimisho ya Mwezi wa Uhamasishaji wa Saratani ya Matiti na yanalenga kuwawezesha wanahabari kuwa mabalozi wa afya kwa jamii.
“Wanahabari wana nafasi kubwa ya kuelimisha jamii kupitia vyombo vya habari na majukwaa ya kidijitali, ili kuongeza uelewa na kupunguza hofu kuhusu ugonjwa huu,” amesema Daulinge.
Ameongeza kuwa endapo saratani ya matiti itagunduliwa mapema, matibabu yake huwa na mafanikio makubwa, hivyo akatoa wito kwa jamii “kuchukua hatua leo na kufanya uchunguzi.”

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi