Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Kampuni inayoongoza katika huduma za mawasiliano na fedha kwa njia ya simu katika nchi 14 barani Afrika, imesisitiza kuwa ushirikiano wa sekta mbalimbali, matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba (AI), na uendelezaji wa vituo vya kuhifadhia data ni nguzo muhimu katika kujenga mustakabali wa kidijitali wa Afrika.
Akizungumza jana katika Kongamano la MWC25 nchini Rwanda,Kigali,Mtendaji wa Airtel Africa,Sunil Taldar amesema maendeleo haya yatachochea mapinduzi ya mawasiliano barani Afrika kwa kubadilisha mtazamo wa teknolojia kutoka kuwa chombo cha kuunganisha watu pekee hadi kuwa nyenzo ya kuongeza thamani na kuibua fursa mpya.
Amesema kuwa Afrika iko tayari kwa hatua inayofuata kutoka kwenye upatikanaji wa huduma hadi kwenye ufanisi na ubunifu.
” Hii inahitaji ushirikiano wa karibu kati ya watoa huduma wanaojenga miundombinu, watengenezaji wa teknolojia, wasimamizi wa sera, wawekezaji, mifumo ya kodi rafiki, na vijana wabunifu wa Kiafrika.
” Kwa pamoja, tunaweza kujenga bara ambalo huduma za intaneti zinachakatwa ndani ya bara, vipaji vinakuzwa kitaifa, na ubunifu unasambazwa duniani kote,”amesema.
Taldar amesisitiza kuwa mustakabali wa kidijitali wa Afrika unahitaji matumizi ya AI ili kuboresha mitandao, kuongeza ufanisi wa huduma, kuboresha uzoefu wa wateja, na kuimarisha usalama wa huduma za fedha kwa njia ya simu.
Amesema ili kufanikisha haya, bara linahitaji mtandao wa vituo vya data vilivyounganishwa kwa nyaya za kasi ya juu, ambavyo vitawezesha upatikanaji wa huduma hata katika maeneo ya pembezoni.
Akitolea mfano, amesema Airtel Africa inawekeza katika vituo vikuu vya data nchini Nigeria na Kenya ili kusaidia mustakabali wa kidijitali wa Afrika. Kampuni pia inatumia AI kubaini ujumbe wa ulaghai (spam), kusajili wateja, na kuboresha matumizi ya nishati safi kwenye minara ya mawasiliano.
Kongamano la mwaka huu la MWC25 Kigali limewakutanisha viongozi wa sekta, wabunifu, na watunga sera, likiwa na lengo la kuangazia namna teknolojia ya mawasiliano ya kidijitali inavyoweza kuharakisha mabadiliko ya bara la Afrika. Rais wa Rwanda, Paul Kagame, alipolizindua rasmi kongamano hilo, amesema.
“Afrika imepiga hatua kubwa kutoka kuwa na miundombinu michache ya mawasiliano hadi kuwa na uchumi unaoendeshwa na teknolojia ya simu za mkononi. Ingawa changamoto bado ni nyingi, pia kuna fursa kubwa za ukuaji endapo tutashirikiana.”amesema
Serikali, sekta binafsi na wadau wengine amesema wanapaswa kuoanisha sera na kuunda mazingira rafiki kwa ubunifu. “Hii itarahisisha mifumo yetu ya data na malipo kuvuka mipaka kwa usalama na kuunganisha uchumi wetu. ,”amesema.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi