March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Urio: Kunduchi miongoni mwa Kata ambayo imepata maendeleo makubwa serikali ya  Awamu ya Sita 

Na Penina Malundo,Timesmajira

Mgombea udiwani wa Kata ya Kunduchi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Michael Urio,amesema Kunduchi ni miongoni mwa Kata ambayo imepata maendeleo makubwa katika serikali ya awamu ya sita ikiwemo kwenye sekta ya afya,Miundombinu na Uwezeshaji wa Kiuchumi kwa wafanyabiashara mbalimbali.

Amesema zaidi ya Sh 310 zimetolewa kwa vikundi mbalimbali vya wananchi kama sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza Jana  Oktoba 19, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mtongani, Kata ya Kunduchi, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Urio amesema kwa  heshima kubwa chama chao  kimefanikisha utekelezaji mkubwa wa miradi katika sekta za afya, elimu, na miundombinu kupitia uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Urio amesema kupitia Mgombea wa Urais kupitia Chama chao Dkt.Samia amehaidi ndani ya siku zake 100 ,amehaidi kwenda kuboresha upatikanaji wa mikopo ya Kinamama,Vijana na Watu Wenyeulemavu .

Amesema mbali na hiyo ndani ya siku hizo 100,Rais Samia anaenda  kurasimisha  biashara za Wajasiriamali wadogo wadogo,Bodaboda,Bajaji na Mamalishe.

“Nitaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wananchi wa Kunduchi, hususan vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, wanawezeshwa kiuchumi kupitia mikopo na mpango wa bima ya afya kwa wote.

“Ndani ya siku 100 zijazo, nitahakikisha kupitia ushirikiano na serikali, biashara zote ndogo ndogo za eneo hilo zinakuwa zimesajiliwa rasmi ili wajasiriamali wadogo waweze kunufaika na fursa za kifedha na mikopo,”amesema 

Akizungumzia  eneo la Kilongawima,amesema tayari kuna  kikundi cha wanawake watano kimepata mkopo wa Sh 100 milioni, ambao umewezesha kuanzishwa kwa kiwanda kidogo cha uzalishaji.

“Eneo la Kondo napo kuna kikundi cha vijana kimepata zaidi ya Sh80 milioni na kimeanzisha kiwanda cha kutengeneza viatu, pia vijana wengine wamepatiwa Sh 130 milioni kwa ajili ya mradi wa utengenezaji wa bidhaa za plastiki.

“Hapa Kunduchi pia tuna kikundi cha wanawake waliopata zaidi ya Sh 30 milioni kwa ajili ya mradi wa kufyatua tofali. Serikali ya Samia imejipambanua kwa vitendo katika kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi,” amesema Urio.

Awali akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkutano huo wa Kampeni,Mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe kupitia chama hicho, Geofrey Timoth, amesema serikali ya CCM itaendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kupunguza michango mashuleni, ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora bila kikwazo cha kifedha.

“Najua wazazi mmekuwa mkikwazwa na michango mashuleni, lakini serikali inachukua hatua kuhakikisha elimu inapatikana bure na kwa ubora zaidi.

“Ndugu zangu wa Kunduchi, sababu za kuwaomba kura tunazo. Ilani ya chama chetu imetekelezwa kwa zaidi ya asilimia tisini. Tunaomba kura zenu ili tukamilishe zile chache zilizobaki,” amesema Timmoth kwa unyenyekevu mkubwa,”amesema.

Timoth amesema Jimbo la Kawe limepata maendeleo makubwa kwenye sekta mbalimbali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambapo imeweza kujenga Hospitali kubwa Mabwepande.

“Tumejengewa pia wodi mbili katika zahanati za Tegeta na Ukuni. Leo hii, vifo vya kina mama wajawazito vimepungua kutoka 19 hadi 9. Haya yote ni matokeo ya uongozi makini wa Dkt. Samia,” amesema.