Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online-Nkasi
Wananchi wa majimbo ya Nkasi Kaskazini na Kusini,wametakiwa kupitia taarifa zilizowekwa kwenye vituo ili kutambua mapema vituo watakavyopigia kura pamoja na kuona mfano wa karatisi za kupigia kura.
Ambapo zoezi la upigaji kura katika uchaguzi mkuu linatarajia kufanyika Oktoba 29,2025, kwa wale wote waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na wana sifa.

Wito huo umetolewa Oktoba 20,2025 na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC), kupitia Msimamizi wa Uchaguzi wa majimbo ya Nkasi Kaskazini na Kusini,George Mwahinda.
Ambapo amesema kuwa vituo vilivyotumika katika zoezi la kuandikisha wapiga kura ndivyo vitakavyotumika kupigia kura siku hiyo.
Mwahinda amesema kwa katika majimbo yote mawili wanatarajia wananchi 214,219 watajitokeza kupiga kura kati yao Nkasi Kaskazini ni 125,078 huku Nkasi Kusini 8,9141.
“Kwa kila kituo cha kupigia kura zimebandikwa taarifa mbalimbali ikiwemo karatasi ya mfano yenye majina na picha za kila mgombea pamoja na nembo ya vyama vyao vya siasa kwa uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani,”amesema Mwahinda.

Sanjari na hayo pia amesema kutakuwa na orodha ya majina ya wapiga kura walioandikishwa na INEC ikiwa ni pamoja na orodha ya wapiga kura walioruhusiwa kupiga kura moja tu ya Rais.
Hata hivyo amesema, siku ya uchaguzi vituo vyote vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni,kwa upande wa vituo vya kupigia kura vya magereza vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 9:00 alasiri.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi