Judith Ferdinand
Kisiwa cha Bezi ni moja ya mtaa unaounda Kata ya Kayenze wilayani Ilemela mkoani Mwanza,ni kisiwa kinachokadiriwa kuwa na wakazi takribani 6,000, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa mtaa huo,ni moja ya eneo linalokabiliwa na changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi.
Vifo hivyo vinatokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa zahanati kisiwani humo,umbali wa kufuata huduma katika vituo vya afya hali inayochangiwa na jiografia ya eneo hilo ambalo ni kisiwa na lipo katikati ya maji.Hivyo wananchi wa eneo hilo hulazimika kutumia mitumbwi au kivuko cha MV.Ilemela kwa ajili ya kufuata huduma za afya ng’ambo.
Ambapo hutumia zaidi ya saa moja na dakika 20 kwa kivuko cha Mv.Ilemela huku kwa mtumbwi ikiwa ni takribani saa sita,ukiachilia mbali gharama ya kukodi ambayo ni laki moja (100,000).

Kutokana na hali hiyo Serikali na wananchi hawajafumbuia macho changamoto hiyo,ambapo wameshirikiana kujenga zahanati kisiwani Bezi ambayo bado haijakamilika.Zahanati hiyo inaelezwa kuwa suluhu ya kudumu ya kuokoa uhai wa mama na mtoto na wananchi kwa ujumla.
Baada ya kutembea takribani saa nne,kutoka katikati ya Jiji la Mwanza mpaka kisiwani Bezi,nikitumia usafiri wa daladala,bodaboda na kivuko cha Mv.Ilemela,kinachotia nanga gati la Kayenze saa 5 na dakika 20,asubuhi.Mwenyeji wangu hapa ni Mwenyekiti wa mtaa wa Bezi,James John,tunatembea takribani kilomita moja na kuniongoza mpaka eneo ilikojengwa zahanati ambayo bado haijakamilika na ujenzi unaendelea.
Mazungumzo yaanza kwa Mwenyekiti wa mtaa wa kisiwani Bezi,James John,anayesisitiza kuwa zahanati ni hitaji kubwa kuliko jambo lolote kisiwani humo.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuwekeza fedha hapa kwenye ujenzi wa zahanati na sisi wananchi kuwekeza nguvu zetu, kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na ukikamilika tunaomba huduma itolewe kwa wakati,”anasema John.
Anasema,katika mradi huo licha ya serikali kutoa fedha lakini wananchi wamejitoa kuhakikisha ujenzi unakamilika ambapo wamebeba takribani tofali 8000 za inchi 6,begani kutoka umbali wa takribani kilomita moja.
Pia anasema baada ya kuapishwa kuwa Mwenyekiti Novemba 29,2024, alikutana na mradi wa ujenzi wa zahanati kisiwani hapo ambao fedha yake ilikuwa tayari imeisha tengwa.
Ambapo miradi ilikuwa miwili mmoja wa zahanati na mwingine wa nyumba ya wahudumu wa afya,lakini wakati huo kwenye mradi wa zahanati ulikuwepo msingi huku nyumba za wahudumu wa afya ulikuwa bado hakijaanza chochote.Hivyo walianza utekekalezaji wa miradi hii yote miwili Januari 31,2025.
John,anasema,kilio cha wananchi ni kuona mradi huo unakamilika haraka ili kunusuru maisha ya wajawazito na watoto wachanga na wananchi kwa ujumla.
Anasisitiza kuwa asilimia 10 ya wananchi kuwekeza katika mradi huo ilikuwa nguvu kazi na wameikamilisha kwa kubeba matofali,mchanga,mawe pamoja na maji huku hatua iliobaki ni Halmashauri kukamilisha,kuleta vifaa tiba pamoja na wahudumu.
“Kutokana na changamoto tulizokuwa nazo huko nyuma kama Mwenyekiti nimeingia nikiwa nazifahamu ikiwemo vifo vitokanavyo na uzazi kwa kukosa huduma ya afya.Ilibidi ni harakishe ujenzi huu ili tuondokane na changamoto hizo, tumetumia muda mchache kuhakikisha tunakamilisha zahanati hii mpaka sasa tumebakiza hatua ya Mkurugenzi kumalizia sehemu iliobaki pamoja na kuweka vifaa tiba,”anasema John na kuongeza:
“Nyumba ya wahudumu wa afya ambayo inabeba familia mbili, utekekalezaji wake umefikia asilimia 90.Katika ujenzi huu wananchi wameshiriki kwa kuchangia nguvu kazi ikiwemo kubeba matofali ya inchi sita kutoka umbali wa takribani kilomita moja mpaka eneo la mradi,maji na mchanga,”.
Kauli hiyo ya Mwenyekiti huyo inaungwa mkono na aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kayenze Issa Mwalukila,wakati akizungumza na Timesmajira Online mara baada ya kufanya ziara Kisiwa cha Bezi,ambacho ni moja ya mtaa unaounda Kata hiyo,anasema wakati anaingia madarakani mwaka 2020 alikuta zahanati ipo katika hatua ya msingi ambao ulikuwa umejengwa na wananchi.
“Nilipeleka mahitaji ya wananchi wa Mtaa wa Bezi serikalini,ambapo tumepatiwa jumla ya milioni 202, kati ya hizo milioni 101 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo na million 101,ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya,ambapo wananchi wameshiriki katika ujenzi wa zahanati hiyo,”amesema Mwalukila.
Anasema,wananchi wa Kisiwa cha Bezi walikuwa wanakabiliwa na changamoto hasa ya kukosa huduma za afya wakati mwingine mjamzito akikaribia miezi ya kujifungua ilimlazimu kuvuka maji kwenda kupanga ili kuwa karibu na huduma,hali ilioongeza gharama za maisha.
“Lakini sasa jibu sahihi linaenda kupatikana hivyo huduma za afya zinaenda kupatikana na watu wa Bezi wanaenda kuishi salama, wajawazito na watoto pia,”anasema Mwalukila.
Ambapo anaeleza kuwa hayo yote yamefanyika kwa ushirikiano wa Serikali,aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,yeye na wananchi ambao wameweka nguvu zao kwa kusomba tofali na kufanya kazi nyingine.
Matarajio ya wananchi wa kisiwa cha Bezi
James Jonh,anasema,wanatarajia baada ya kukamilika kwa zahanati hiyo ifunguliwe na kuanza kutoa huduma huku akisisitiza kuwa itakuwa maajabu zahanati ikamilike lakini kufunguliwa na kuanza kutoa huduma kukachelewa.
“Sisi tunaiomba Serikali kadri wananchi walivyojitahidi kukamilisha mradi huu kwa uharaka, basi eneo lililobaki limaliziwe na kuifungua kwa haraka,kuleta vifaa tiba na wahudumu wa afya ili iwe na tija kwa wananchi wa Bezi na kuokoa maisha ya watu,”.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kisiwa cha Bezi,Esther Warioba,anasema wamama kisiwani humo wakibeba mimba wamekuwa wanawaza kuwa watakufa au vipi na ilifikia kipindi uongozi wa mtaa ulitoa tamko kuwa mjamzito akifikisha miezi nane aende kwao au akapange karibu na kituo cha kutolea huduma.
“Tunamshukuru Mungu hata kwa jitihada ya ujenzi wa zahanati hii ambayo imebaki kidogo kukamilika.Tumeteseka mtu akibeba mimba anaanza kuwaza kuanzia mimba ina mwezi mmoja mpaka miezi tisa,sijui nitakufa,sijui sitakufa,Mungu anasaidie wengine wanapona wengine wanafariki,”anasema Esther.
Baadhi ya wananchi wa kisiwani Bezi akiwemo,Novatus Cheusi,anasema matarajio yao baada ya zahanati hiyo kukamilika na kuanza kutoa huduma vifo vingi vya wajawazito na watoto wachanga vitapungua,kwani mtu akianza kuhisi uchungu atapata huduma mara moja na haraka.
Cheusi,anasema anatamani zahanati hiyo ikamilike haraka ili wajawazito waanze kuhudumiwa na kupata huduma za kliniki kwa usahihi, kupunguza gharama na mwendo wa kufuata huduma za afya nchi kavu.
“Mara nyingi wanawake kisiwani humu wanapata uchungu usiku pindi usafiri unapokuwa umeisha ondoka,hiyo imekuwa changamoto tumeshuhudia vifo vya kina mama wakati wa kujifungua. Kitendo cha kupata zahanati hapa endapo itakamilika itatusaidia,na kuwa na mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya wananchi hususani ya mama na mtoto vile vinavyotokana na uzazi,”anasema Cheusi.

Kwa upande wake Hassani Nagabona,anasema anamatumaini baada ya zahanati kukamilika kutakuwa na huduma bora za afya hasa kwa wajawazito,ambao kwa sasa wanalazimika kutumia muda mrefu kwenda kupata huduma ya kliniki katika kituo cha afya Kayenze,adha ya usafi,muda pamoja na gharama.
“Kupitia zahanati hii wataweza kupata huduma sehemu muafaka na kwa muda mfupi,hivyo ni matumaini mamkubwa ya uhai wa mama na mtoto.Pamoja na jamii ya uvuvi kuweza kupanga uzazi kwa sababu watapata elimu ya njia ya uzazi wa mpango ambayo itakuwa karibu,”anasema Nagabona.
“Tunachoshukuru sasa Serikali imejitahidi kutuletea zahanati ingawa bado haijakamilika na kuanza kutoa huduma, lakini matumaini yetu itatufuta machozi na kuondoa vifo vitokanavyo na uzazi.Changamoto ni wajawazito na watoto wachanga kupoteza maisha wakati wa kujifungua,tumepoteza ndugu zetu na rafiki zetu kwa kukosa zahanati,”anasema Pendo Waryioba mmoja wa wakazi wa Kisiwa cha Bezi.
Naye Julius Ntenganija, anasema vifo vya wajawazito vilikuwa vingi ndio sababu ya kuomba zahanati ijengwe mtaani kwao.
“Matarajio yetu baada ya kukamilika kwa ujenzi wa zahanati hii ni kupunguza vifo vya mama na mtoto na kutoa huduma ya afya kwa wananchi wote,kwani tulikuwa tunatumia takribani saa tatu kufuata huduma za afya ng’ambo na gharama ni kubwa,”anasema Ntenganija.
Nini mipango ya Serikali ya kuboresha huduma za afya kisiwani Bezi
Kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Dkt.Maria Kapinga,anasema ipo mipango ya muda mfupi na mirefu ya kuboresha huduma za afya kisiwani Bezi.
Dkt,Kapinga,anasema kupitia mpango wa TASAF–OPEC 4, ujenzi wa zahanati katika Kisiwa cha Bezi umeanza,
jambo ambalo linatarajiwa kuwa suluhisho kubwa kwa changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakabili wakazi wa eneo hilo ikiwemo vifo vitokananvyo na uzazi.
“Ujenzi huu utakapokamilika, utasaidia kupunguza vifo vya uzazi kisiwani humo kwa kutoa huduma ya karibu kwa mama na mtoto.Kuwezesha huduma za chanjo, kliniki za wajawazito na watoto wachanga kufanyika mara kwa mara,”anasema Dkt.Kapinga na kuongeza:
“Pia itasaidia kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa jamii yote ya kisiwa,uwekezaji wa mafunzo kwa wahudumu wa afya wa jamii ili kuimarisha huduma hata kwa wale walioko mbali na kituo,”.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,Aprili 9, 2025,alipowasilisha hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2025/2026 Bungeni jijini Dodoma,alisema vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2020 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 Februari, 2025.
Ambapo vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano navyo vimepungua kutoka 67 mwaka 2020 hadi 43 Februari, 2025,hii ni kutokana na jitihada za kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini, unaofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi.
“Jitihada hizo zimewezesha kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma za afya kutoka vituo 8,458 mwaka 2020 hadi vituo 9,826 Februari, 2025,hospitali zinazotoa huduma ya magonjwa ya dharura zimeongezeka kutoka saba mwaka 2020 hadi 116 mwaka 2025.
“Pia, vituo vya kutolea huduma za afya vyenye majengo ya mama na mtoto vimeongezeka kutoka 6,081 mwaka 2020 hadi 7,397 Februari, 2025,”.

–
–

More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati