March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DG VETA azungumzia umuhimu wa mafunzo ya ufundi kwa vijana

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online , Mbeya

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amesema kuwa mafunzo ya ufundi stadi ni njia muafaka ya kuwawezesha vijana kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Y.

CPA Kasore amesema hayo alipofanya ziara katika Chuo cha VETA Mkoa wa Mbeya, ambacho ni miongoni mwa vyuo vya muda mrefu vilivyoanzishwa kwa lengo la kutoa ujuzi wa vitendo kwa vijana katika fani mbalimbali ili kuwawezesha kupata ujuzi utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza mara baada ya kutembelea karakana za chuo hicho zikiwemo Carpentry and Joinery, Auto-Electrical, Plumbing and Pipe Fitting, pamoja na Urembo na Ususi, alisema kuwa VETA inaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia.

“Lengo ni kuhakikisha kuwa tunatoa mafunzo bora, yanayokwenda na wakati. Mathalani, katika karakana ya Auto-Electrical, sasa tunafundisha vijana kutumia vifaa vya kisasa kama ‘diagnostic machines’ ili waweze kutambua na kushughulikia changamoto za magari ya kisasa yanayotumia mifumo ya umeme na kompyuta,” amesema Kasore.

Ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya teknolojia, VETA pia imeanza kufundisha teknolojia ya magari ya umeme (hybrid vehicles), ili kuhakikisha vijana wanakuwa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la sasa na la baadaye.

CPA Kasore amèsema VETA inaendelea kupanua wigo wa mafunzo kwa kuanzisha fani mpya kama Visual and Performing Arts kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Bodi ya Filamu. Mafunzo hayo yanawalenga wasanii, waimbaji, waigizaji na watu wanaofanya kazi za ubunifu kwenye majukwaa.

“Ujuzi haumaanishi uinjinia peke yake. Hata vipaji kama uigizaji, muziki na sanaa za maonyesho ni ujuzi unaoweza kuwasaidia vijana kupata kipato na kushiriki katika uchumi wa nchi,” amesema.

Amebainisha kuwa VETA inalenga kuwapa Watanzania ujuzi unaoendana na sera mpya ya elimu ya mwaka 2023, inayolenga kujenga fikra tunduizi, ubunifu, na uwezo wa kushindana kitaifa na Kimataifa katika soko la ajira.

Aidha CPA Kasore ameeleza kuwa serikali, kwa kushirikiana na VETA, imeanzisha zaidi ya vyuo 80 nchini katika kipindi cha miaka minne iliyopita, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kusogeza huduma karibu na wananchi.

“Rais alitoa shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vipya 65, ambapo kimoja ni cha Mkoa wa Songwe, na vingine 64 viko katika wilaya mbalimbali. Ujenzi unaendelea ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata nafasi ya kujifunza ujuzi unaohitajika katika eneo lake,” amesema.

Alitoa mfano wa wilaya zinazojishughulisha na kilimo au madini, ambapo VETA imejielekeza kutoa mafunzo yanayohusiana moja kwa moja na shughuli hizo, ikiwa ni pamoja na kuongeza thamani ya mazao au bidhaa za madini.

Akieleza kuhusu ushirikiano wa kimkakati, CPA Kasore alisema VETA inashirikiana kwa karibu na waajiri, wamiliki wa viwanda na wadau wa maendeleo, ili kuhakikisha mitaala ya mafunzo inalingana na mahitaji ya soko la ajira.

“Tarehe 17 Oktoba mwaka huu, tutakuwa na mkutano mkubwa baina ya VETA na wadau mbalimbali wa viwanda ili kujadiliana namna bora ya kuimarisha ubora wa mitaala, uwezo wa walimu, na kuhakikisha mhitimu anakuwa na ujuzi sahihi unaotakiwa,” amesema.

CPA Kasore pia alieleza kuwa VETA inaendeleza miradi ya kuwajumuisha vijana walioko kwenye mazingira magumu na wenye mahitaji maalum kwa kuwajengea miundombinu rafiki na kutoa mafunzo maalum. Kila mwaka, kati ya vijana 1,000 hadi 1,500 hufikiwa kupitia programu hizo.

“Tuna hakikisha hata wale wenye changamoto za kimazingira au kiafya wanapata fursa ya kujifunza. Tumeweka miundombinu rafiki kwenye vyuo vyetu, na tunaendelea kushirikiana na halmashauri kuhakikisha vijana hawa wanafikiwa,” amesema.

CPA Kasore amesisitiza kuwa mafunzo ya ufundi stadi ndiyo suluhisho la changamoto za ukosefu wa ajira kwa vijana nchini, na kwamba VETA itaendelea kuhamasisha vijana kutumia fursa zilizopo kujifunza ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa, kujiajiri na hata kuajiri wengine.