Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online , Mbeya
KATIBU Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Ahmed Said, amezitaka taasisi za dini, hususan vyuo vinavyoendeshwa na taasisi hizo, kuweka utaratibu wa kuwasaidia vijana kupitia huduma za ushauri nasaha (counseling) ili kuwakinga dhidi ya changamoto za msongo wa mawazo na matatizo ya afya ya akili.
Akizungumza jijini Mbeya wakati wa kufunga Kongamano la Kitaifa la Vijana, Zena amesema kuwa changamoto za kisaikolojia kwa vijana zimeongezeka kwa kasi, na zinachangiwa na mambo mbalimbali, ikiwemo presha ya maisha, mitazamo ya kijamii na matumizi ya mitandao ya kijamii.
“Taasisi za dini zina nafasi kubwa ya kusaidia vijana. Vyuo vinapaswa kuwa na watu wa ushauri nasaha ili kuwapa elimu mapema kabla hawajakutana na msongo wa mawazo. Tunapozuia matatizo kabla hayajakomaa, tunaokoa kizazi,” amesema
Zena amewahimiza vijana kuwa makini katika kila uamuzi wanaoufanya katika maisha, kwa kuwa kila hatua wanayochukua ina matokeo yake. Alisema vijana wanapaswa kuwa na mizani ya maadili katika kufanya maamuzi, na kuepuka vitendo vinavyoweza kuwa na madhara kwao au kwa jamii.
“Kila unachokifanya, hakikisha si jambo baya. Fikiria kabla ya kutenda. Maamuzi mabaya leo, yanaweza kuharibu maisha yako ya baadae,” amesisitiza.
Akielezea hali ya afya ya akili miongoni mwa vijana, Zena alieleza kuwa baadhi yao wameanza kutumia dawa za kulevya, bangi, gundi na hata dawa za usingizi za hospitali ili kukabiliana na changamoto za maisha hali inayohatarisha maisha na mustakabali wao.
Amesema ni muhimu jamii kutoa msaada wa kihisia kwa vijana, kuwapa nafasi ya kuzungumza matatizo yao, na kuwahamasisha kutafuta msaada wa kitaalamu badala ya kutafuta suluhisho kupitia njia za hatari.
Aidha, amewaonya vijana dhidi ya kutumia mitandao ya kijamii kama kipimo cha mafanikio. Alisema vijana wengi hujikuta wakipatwa na msongo wa mawazo kwa kujilinganisha na maisha yanayooneshwa mtandaoni, ilhali ukweli wa maisha hayo haujulikani.
“Unapoangalia mafanikio ya watu mitandaoni, kama nyumba au magari, na wewe unaona huna hivyo – unapata msongo wa mawazo. Lakini wengi wanaoonesha vitu hivyo si vyao, ni maigizo tu. Usiishi maisha ya mtu mwingine,” amesema.
Amewataka vijana kutumia mitandao kwa ajili ya maarifa, mawasiliano yenye tija, na sio kufuatilia maisha ya watu ambayo yanajenga presha na kushusha thamani binafsi.
Katika hotuba yake, Zena pia alizungumzia athari za kupokea taarifa mbaya kila wakati, hasa kuhusu migogoro ya kimataifa na majanga yanayoripotiwa kupitia vyombo vya habari au mitandao. Alisema tabia ya kufuatilia taarifa za huzuni au vurugu kila wakati inaweza kuchochea hali ya msongo wa mawazo kwa mtu asiyetambua athari zake.
“Kuna watu ambao hupenda kuangalia habari mbaya kila siku; kwao hizo ndizo taarifa muhimu. Watu hawa wana uwezekano mkubwa wa kuishi kwenye hali ya huzuni na msongo. Tujifunze kuchuja taarifa tunazopokea,” ameongeza

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi