



Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online ,Mbeya
DAKTARI wa Mifupa kutoka Taasisi ya MOI, Dkt. Angela Mlingi, amesema kuwa watu wengi wanakumbwa na matatizo ya mifupa hususan mgongo na nyonga, lakini kutokana na uelewa mdogo, wamekuwa wakisita kufika hospitalini kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yaliyofanyika mkoani Mbeya, Dkt. Mlingi amesema kuwa hadi sasa wamewahudumia jumla ya wagonjwa 472, ambapo wengi wao walikutwa na matatizo yanayohusiana na mgongo na nyonga.
“Katika wagonjwa tuliowaona, tumewashauri baadhi kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa huduma zaidi. Hata hivyo, takriban wagonjwa 40 walihitaji rufaa ya moja kwa moja kwenda MOI kwa matibabu ya kitaalamu zaidi,” alisema Dkt. Mlingi.
Dkt. Mlingi alisema kuwa changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu umuhimu wa kutafuta huduma za afya mapema. Alisema baadhi ya watu huendelea kuvumilia maumivu kwa muda mrefu badala ya kufika hospitalini kwa uchunguzi wa awali.
“Tunawasihi wananchi kutafuta huduma za afya mapema. Ni bora ukapime na kugundua huna tatizo, kuliko kusubiri hadi hali iwe mbaya. Maumivu yakianza si vyema kuyapuuzia,” alisisitiza.
Katika kuboresha huduma za afya mikoani, Dkt. Mlingi alieleza kuwa MOI imewajengea uwezo madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa kuwapa mafunzo ya kitaalamu, hatua inayowezesha hospitali hiyo kutoa huduma nyingi za awali kwa wagonjwa wa mifupa bila ulazima wa rufaa kwenda Dar es Salaam.
“Tunaendelea kushirikiana kwa karibu na hospitali za mikoa kama Mbeya. Madaktari hapa sasa wana ujuzi wa kutosha kushughulikia baadhi ya changamoto za mifupa, jambo ambalo linapunguza msongamano wa wagonjwa MOI,” amesema.
Aidha, Dkt. Mlingi ametoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kudhibiti matatizo ya mifupa, na vilevile kutafuta huduma za kitabibu pindi wanapohisi dalili zozote.
“Tumeendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa mazoezi. Lakini pia tumegundua kuwa wagonjwa wengi wanajua wanaumwa, lakini kupata huduma hospitalini ni changamoto – wengine kwa sababu ya kutojua wapi pa kuanzia,” amesema.
Dkt. Mlingi amesisitiza kuwa afya bora huanza na uamuzi wa kufuatilia hali ya mwili, hivyo ni vyema kila mtu akajenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara na kupata ushauri wa kitaalamu.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina