March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rc.Chalamila azindua programu ya Konekt Umeme,Pika kwa Umeme

Na Penina Malundo,Timesmajira

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila leo Octoba 09,2025 amezindua programu ya Konekt Umeme, Pika kwa Umeme iliyobuniwa na TANESCO katika viwanja vya Mwembe yanga wilaya ya Temeke.

Programu ya Konekt Umeme, pika kwa umeme ni gharama nafuu, inaufanisi mkubwa, pia umeme unaotumika ni kidogo sana ukilinganisha na nishati zingine.

RC Chalamila amepongeza Wizara ya Nishati, na TANESCO na wadau wote wa maendeleo kwa kuja na wazo hili bunifu lenye lengo la kuongeza upatikanaji wa Nishati safi ya kupikia kwa Watanzania. “Mpango huu ni mwanzo wa zama mpya katika historia ya huduma za umeme nchini unaounga mkono juhudi ya Rais Dkt Samia Suluhu katika matumizi ya nishati safi”.

Kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya umeme kupikia unaifanya jamii ya kitanzania kwenda kwenye viwango bora vya maisha.

Vilevile RC Chalamila amesema ni ukweli usiopingika umeme ni hitaji muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi lakini maendeleo ya mtu mmoja mmoja.

Aidha kwa upande wa Mtendaji mkuu wa TANESCO, Lazaro Twange amesema Tanzania kupitia wizara ya Nishati, TANESCO imetangaza rasmi mpango wa kitaifa wa Nishati (Energy Compact) wenye lengo la kuunganisha wateja milioni 8.5 ifikapo 2030 sawa na wateja milioni 1.7 wapya kila mwaka hivyo uzinduzi wa programu ya Konekt Umeme, Pika kwa umeme umefanyika muda muafaka.

Amesema shirika hilo limeanza kusambaza majiko ya umeme kwa mkopo siyo tu kwa wafanyakazi wake, bali sasa kwa wananchi wote kupitia mpango wa kulipa kidogo kidogo kupitia bili za umeme.

Twange amesema kuwa mpango huo umeondoa kikwazo cha gharama za awali na kufungua milango kwa kaya nyingi kuingia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Sanjari na hilo amesema mpango huu unatoa fursa kwa mteja kupewa jiko wakati wa kuunganishiwa umeme kisha analipa kidogo kidogo kupitia mfumo wa token hivyo familia nyingi sasa zitaweza kupika kwa ufanisi na kwa gharama nafuu.

RC Chalamila amegawa majiko ya Nishati safi ya umeme kwa wananchi mbalimbali na kuwataka kuwa mabalozi kwa jamii ya kitanzania.