Allan Vicent na Jumbe Ismaily,TimesMajira Online, Igunga
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mgombea udiwani katika Kata ya Sungwizi Tarafa ya Simbo wilayani Igunga mkoani Tabora, Katambi Sospeter amejikuta katika wakati mgumu baada ya kudodosha kibuyu cha dawa za kienyeji alipokuwa akiingia kwenye ukumbi wa kupigia kura za maoni katika Shule ya Msingi Sungwizi.
Tukio hilo limetokea Julai 25, 2020 muda wa saa 5:38 asubuhi ambapo mgombea huyo wakati akijaribu kupanda ngazi ili kuingia katika jengo hilo kibuyu hicho chenye dawa kilidondoka kwa bahati mbaya kutoka kwenye mfuko wake wa suruali mbele ya wajumbe.
Wajumbe wa mkutano huo walipoona tukio hilo walimwambia kuwa ameangusha kifaa chake ambapo alishikwa na bumbuwazi na mmoja wa wajumbe hao Therezia Bleki alikiokota na kumkabidhi ambapo askari mgambo wawili waliokuwa wakilinda eneo hilo walimtoa nje ili kumhoji.
Sospeter alikiri kuwa kibuyu hicho ni cha kwake na kuongeza kuwa kwenye familia yao wamezaliwa mapacha hivyo kiutaratibu wanatakiwa kutembea na kibuyu cha dawa wakati wote.
Aidha, alipotakiwa kukikabidhi kwa walinzi (mgambo) ili asiingie nacho ukumbini aligoma, na baada ya majadiliano yaliyochukua takribani dakika 30 bila mafanikio mgombea huyo aliwatoa pembeni mgambo hao pamoja na mwandishi wa habari na kuomba wamruhusu aingie nacho kwa ahadi ya kuwapatia fedha kidogo.
Aidha, baada ya juhudi zake kugonga mwamba aliamua kukipeleka nyumbani na kurudi kupiga kura za maoni.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Sungwizi, Emmanuel Mpya alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alionesha kushangazwa na mgombea huyo huku akibainisha kuwa ni kutokujiamini tu, huku akimtaka kutorudia tabia hiyo
Baada ya sakata hilo zoezi la upigaji kura liliendelea ambapo Njeri Ibrahim alipata kura 21, Katambi Sospeter kura 22 huku diwani aliyemaliza muda wake Matikito Gaspar akiibuka kidedea kwa kura 62.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani