December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima waishukuru Serikali kuimarisha miundombinu ya usafirishaji

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Momba.

CHANGAMOTO ya maeneo korofi ya barabara ya Igamba – Msangano hadi Chitete yenye urefu wa kilometa 87.4 imetatuliwa na kufanya barabara hiyo kupitika kwa kipindi chote cha mwaka, ikiwemo ujenzi wa daraja la mto Nkala.

Kutoakana na kutatuliwa kwa changamoto hiyo wakazi wa vijiji vya kata za Chitete na Msangano katika Wilaya ya Momba, Mkoani Songwe, wameishukuru serikali kupitia Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Mkoa wa Songwe kwa kufanikiwa kuimaliza.

Wananchi hao kutoka katika bonde maarufu kwa kilimo cha mpunga la Msangano ambako pia kuna skimu kubwa za umwagiliaji, wamesema daraja hilo lililojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 527 limerahisisha shughuli za usafirishaji wa mazao yao kwenda kwenye masoko.

Wametoa shukurani hizo hizo hivi karibuni katika mahojiano maalum na mwandishi wetu yaliyolenga kujua namna serikali ya awamu ya sita ilivyofanikiwa kutatua changamoto mbalimbali ndani ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan akiwa madarakani.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Chilulumo, Henricko Sinkala, akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, aliipongeza serikali ya kwa namna ilivyoweza kumaliza changamoto ya daraja hilo ambapo zamani lilikuwa likisababisha maafa kwa watu kupoteza maisha, ikiwemo mifugo yao kusombwa na maji.

Naye, Gerald Emanuel, Mkazi wa Chitete amesema kukamilika kwa daraja hilo kwa lkiasi kikubwa imesaidia wao kusafirisha mazao yao kutoka kijijini hadi kwenyhe masoko yenye bei nzuri katika miji ya Mlowo na Tunduma.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga, alisema daraja hilo la kudumu limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 527 na Mkandarasi mzawa wa kampuni ya Byam kutoka Jijini Dar es salaam.

“Daraja hili la mto Nkala ni draja ambalo kwa watu wa Momba upande wa Chitete limesaidia sana kwani kuna jumla ya vifo saba viliripotiwa kutokea wakati kukiwa na daraja dogo na baada ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutupatia fedha na tumefanikiwa kujengas daraja kubwa na la kudumu ambalo sasa limemaliza changamoto zote za usafirishaji, ikiwemo madhara kama vifo” alisema Mhandisi Bishanga.

Alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 87.4 ni muhimu kwa usafirishaji wa mazao ya mpunga na kwenda kwenye masoko yaliyopo katika miji ya Mlowo na Tunduma.

Aidha, Mhandisi Bishanga alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia madarakani, Tanroads Mkoa wa Songwe imepokea wastani wa shilingi bilioni 40 kama fedha za matengenezo kwa barabara za Mkoa, barabara Kuu pamoja na madaraja.