December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

6,000 wawezeshwa Bima ya Afya

Na Esther Macha, Timesmajira, Online, Mbeya

Wananchi 6,000, mkoani Mbeya wamewezeshwa bima za afya bure na taasisi ya Tulia Trust kupitia Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt.Tulia Ackson ikiwa ni jitihada za kuunga mkono serikali katika sekta ya afya.

Akiwakabidhi bima hizo wananchi hao leo
Naibu Waziri Mkuu,Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko,amesema kuwa kitendo kilichofanywa na Dkt.Tulia kutoa bima za afya bure kwa wananchi mkoani Mbeya ni jambo la ibada ambalo lengo ni kupata huduma bora za afya na kusema kwamba hilo ni somo kwa walio wengi hususani Wabunge waliochaguliwa.

Sanjari na hayo Dkt.Biteko amesema kwamba licha ya Dkt.Tulia kuwakilisha wananchi wa Mbeya Bungeni lakini bado anawakilisha nchi duniani hivyo imani yake kubwa kwa watu wa Mbeya watailinda heshima yake.

“Sisi Wabunge wenzako na tuliopo serikalini utakapokuwa unasimamia shughuli za Bunge tutahakikisha kila linalowezekana kuondoa changamoto zote zilizopo katika Jimbo hili tunaziondoa kabisa kwani itakuwa ajabu sana umepata heshima ya kidunia bado uendelee kuhangaika na changamoto ndogo ndogo za zahanati,”amesema Dkt.Biteko.

Kwa upande wake Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini ambaye pia ni Rais umoja wa Mabunge Duniani, Dkt.Tulia Ackson amesema kuwa bima za afya ambazo zinatolewa kwa wananchi pamoja na kwamba hawana vyama wanaenda kupata huduma ambako CCM imefanya kazi nzuri.

Dkt. Tulia amesema kuwa, bima hizo zinazotolewa na Taasisi ya Tulia zitawawezesha wananchi kupata matibabu hadi ngazi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Taasisi ya Tulia imekuwa na utaratibu wa kutoa bima hizo za afya kwa Wazee, Watu wenye ulemavu na kaya zenye uhitaji ambapo kutoka mwaka 2019 hadi sasa jumla ya kaya 2670 zimefaidika huku idadi ya wananchi wakiwa ni 16,020 na zoezi hilo linaendelea.

“Kuhusu hospitali ya wazazi Meta mnajua namna ilivyokuwa huko nyuma sasa hivi huduma zimekuwa bora zimeingia zaidi ya bilioni 17 .3 jengo limekamilika,wanasubiri Rais Samia aje kunzindua rasmi maana tayari kumeboreshwa vizuri,”amesema Dkt.Tulia.

Chifu Mkuu wa mkoa wa Mbeya Rocket Mwashinga,ameomba kuwe na dirisha la wazee kwani wanapata shida pindi wanapofika kupata huduma za matibabu katika hospitali na vituo vya afya pamoja na zahanati na kuomba wazee na watoto waheshimiwe na kuthaminiwa .