December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

52 wahitimu mafunzo ya Kilimo cha Utaalam TADB

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imefunga mafunzo ya Kilimo cha Kitaalam, yalioendeshwa na BOT Academy kwa lengo la kuzalisha wataalam wa kutosha katika sekta hiyo.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwa na wataalam ambao watasaidia kutoa mikopo katika sekta nzima ya kilimo.

Hayo aliyasema leo na Kaimu Mkurugenzi Muendeshaji wa Benki ya Kilimo, Dkt. Kaanael Nnko wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Odwizungwa uliopo Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam, mara baada ya kufunga mafunzo hayo.

Dkt. Kaanael amesema, katika mafunzo hayo walikuwa na wahitimu wapatao 52 kutoka benki washirika 20 ambao wameshiriki. Lakini pia kwa bahati ya pekee wamepata washirika wawili kutoka nchini Burundi.

“Tunashukuru sana Benki Kuu ya Tanzania, kupitia BOT Academy ambao ndio wameendesha mafunzo haya na pia washirika wetu wengine ambao Chuo Kikuu cha Kilimo (Sokoine Agriculture University), na Chuo Kikuu cha SAUT, ambao wamekuwa washirika wetu wazuri.

“Tangia kutengeneza ‘Program’ mpaka kufundisha kuhakikisha wahitimu wetu wa kwanza wamehitimu na wamepata mafunzo. ndio maana leo mmeshuhudia wakipata vyeti vyao,” amesema Dkt. Kaanael.

Aidha, amesema lengo lingine la mafunzo hayo ni kuhakikisha wakulima wengi wanafikiwa katika mikoa yote ndio maana benki ya kilimo imekuwa ikiendesha mafunzo kama hayo.

Amesema, mpaka sasa mfuko wa garantee ambao unaitwa SCGS umeweza kudhamini mikopo takribani Bil. 270, ambapo mikopo yote imepitia benki washirika.

“Mpaka hivi tunavyoongea tumeweza kuwafikia walengwa ambao wakulima wa moja kwa moja 24,000, kwa hiyo ukiangalia tunapoanza mafunzo haya tayari tuna mafanikio ambayo tunaweza tukayasema.

“Na Tunaamini kwa haya mafunzo na hawa washirika ambao wameshiriki tukipata nafasi ya kukutana nao tena tutakuwa na mafanikio zaidi,” amesema Dkt. Kaanael.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo cha Benki ya Tanzania, kilichopo jijini Mwanza, Dkt. Ephrem Kasanguti amesema majukumu makubwa walionayo ni kuelemisha mabenki na taasisi za fedha pamoja na wafanyakazi wa Benki Kuu juu ya taaluma mbalimbali.

“Katika kutimiza majukumu yetu chombo cha BOT kina jukumu la kuelimisha na kuchangia dhima na Dira ya Benki Kuu, tulipewa kazi na Benki ya Kilimo (TADB) ya kutengeneza ‘Program’ kwa ajili ya wakulima wadogowadogo.

“Hasa kwa lengo la kuelimisha mabenki ambao wana maafisa mikopo ili waweze kutoa mikopo ambayo italipika kwa sababu hizi fedha za umma lazima zilipike na ziwe na matokeo mazuri ya kilimo katika nchi yetu.

“Tukatengeneza hiyo Program, ambayo ndio hasa leo tumehitimisha kwa kutoa vyeti kwa wahitimu kwa kushirikiana na Chuo cha Kilimo SUA pamoja na SAUT.

“Hii ni kozi yetu ya kwanza, tuanazo kozi zingine ngazi Stashahada na ‘Postgraduate’, zipo kozi zingine zinakuja kwa hiyo tuna mafanikio makubwa katika Chuo chetu kwa ajili ya kutimiza dhima na Dira ya Benki Kuu ya Tanzania,” amesema Dkt. Kasanguti.

Kwa upande wake mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo Salvatory Sylevester ambaye ni Meneja Mahusiano Kilimo Biashara kutoka CRDB, amesema mafunzo hayo yamewasaidia sana kufungua mtazamo wake kuhusu Kilimo.

Amesema, kwa muda mrefu taasisi za kifedha zimekuwa zikiangalia Kilimo ni sehemu au sekta ya nchi ambayo ina viashiria vingi hatarishi, kwa hiyo mafunzo hayo yamewasidia sana kuwafungua na kuangali fursa zilizoo kwenye kilimo na kutoa mikopo yenye tija.