Na Allan Ntana, Tabora
WATU 5 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Tabora kuhusiana na mauaji ya askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) MT.117342 PT Samwel Machugu Anton (28) wa kikosi cha 262 Milambo aliyeuawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana Mkuu wa wilaya ya Tabora mjini Komanya Kitwala ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani hapa alisema kuwa watu hao wamekamatwa kutokana na msako mkali unaoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi Mkoani hapa kufuatia mauaji ya askari huyo yalitokea Machi 30 mwaka usiku maeneo ya Kidatu B Kata ya Ipuli katika Manispaa ya Tabora.
Alisema kuwa majina ya watuhumiwa waliokamatwa kwa tuhuma hizo yamehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi.
Alisema kuwa askari huyo alikutwa na mauti baada ya kuachana na wenzake aliokuwa nao kwenye doria ya ulinzi shirikishi wa Mtaani kwake na kwamba akiwa njiani kurejea nyumbani ndipo alikutana na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni vibaka ambao walimpiga mara tatu na kitu chenye ncha kali kichwani na kupelekea kifo chake.
Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa
Jeshi hilo kwa kuwafichua wahalifu wote katika maeneo yao huku akiwataka
kutojichukulia sheria
mkononi dhidi ya wahusika wa mauaji ya askari huyo pamoja na watuhumiwa wa
matukio mengine kwa kuwa sheria inachukua mkondo wake kwa mujibu wa taratibu na
sheria kwa watakaobainika.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wakazi hao kuwa watulivu kwa kuwa Jeshi hilo limejipanga vizuri na litafanya doria kwa masaa 24 katika Mitaa yote ili kupambana na wahalifu na kudhibiti vitendo vyote vya kihalifu na kwamba wanapopata taarifa za uhalifu wampigie kwa namba 0713 944 580 au wampigie Mkuu wa Polisi wilayani humo( OCD) ASP George Wilbad Bagyemu kwa namba 0715/0787/0755 284 244 iliwachukue hatua mara moja.
Aidha Komanya aliwataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume na sheria kuzisalimisha kituo cha Polisi kuanzia Aprili 6 mwaka huu 2020 hadi Mei 4 mwaka huu 2020 na wale wanaomili kihalali wazipeleke kuhakikiwa na kwamba baada ya muda huo kupita watakaobainika kutozipeleka watakamatwa na kukishwa mahakamani.
Alisema lengo la zoezi hili ni kudhibiti matukio ya kihalifu
yanayowezakutokea kwa kutumia silaha hizo na kwamba watafanya msako mkali
kuwabaini watu wote wanaomiliki silaha kinyume na sheria na kuwachukulia hatua
kali na kuhakikisha wanakomesha na kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya
silaha hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo (OCD) ASP George Wilbard Bagyemu
alivitaka vikundi vyote vya ulinzi shirikishi kufanya kazi zao kwa kushiriana
na Polisi Kata, Ofisa Mtendaji Kata,Mkuu wa kituo kikuu cha Polisi na yeye
mwenyewe ili kupata maelekezo muhimu ya kiutendajikazi na kuleta ufanisi zaidi.
Alikiri kuwa vikundi hivyo huko nyuma vililegalega kufanya kazi,vilikuwa havifuati taratibu na maelekezo na vilikosa ushirikiano wa viongozi hao kutokana na kufanya kazi kienyeji na kupelekea kukosa nguvu ambapo kwa sasa wameviimarisha na kuvipatia maelekezo muhimu pamoja na vitendea kazi kama tochi,betri na filimbi ili vifanyekazi kitalaamu.
More Stories
Walimu elimu ya lazima watatakiwa kuwa wabobezi kwenye masomo wanayofundisha
Wahakikishiwa usalama siku ya kupiga kura
CCM inabebwa na kazi nzuri za Rais Dkt. Samia-Makalla