November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tazama wanufaika wa TASAF wanavyojiinua kupitia sekta ya kilimo

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Mbeya

BAADHI ya wanufaika wa Mpango wa kunusuru  Kaya masikini  (TASAF) wameonyesha kufurahishwa na huduma hiyo ambayo imewazesha kujiinua kiuchumi kwa kufanya shughuli za kilimo.

Wakizungumza katika maonyesho ya Wakulima Nane Nane jijini Mbeya wanufaika hao wamesema,mpango huo ni mzuri kwa watu wasiokuwa na uwezo huku wakiiomba Serikali iendelee kutoa huduma hiyo kwa wananchi wake.

Sarah Japhet mkazi wa Mbeya amesema,kabla ya kuingia katika mpango huo alikuwa na hali nguu kimaisha na alikuwa akiishi katika nyumba ya nyasi lakini baada ya kuingia katika mpango huo ameweza kujenga na kuiezeka kwa bati .

Mnufaika mwingine Enos Ngabo amesema baada ya kuingia katika mpango wa TASAF ,sasa analima mazao kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam na hivyo kuzalisha kwa tija.

“Kabla ya kuingia TASAF nilikuwa siwezi hata kununua mbolea,sikuweza kumudu vibarua wa kunisaidia shambani lakini sikuweza hata kulipia maji,”amesema Ngabo

Baadhi ya wanufaika wa TASAF wakiwa katika maonyesho ya Wakulima Nane Nane katika viwanja vya Joihn Mwakangale jijini Mbeya wakiuza bidhaa zao walizolima kupitia mpango wa TASAF.

Amesema,kwa sasa yeye pamoja na wenzanke ni kioo katika jamii ambao wanapaswa kuigwa katika matumizi ya fedha hizo za TASAF.

Amewaasa wanufaika wengine kuhakikisha wanatumia fedha katika shughuli za kujiingizia kipato kupitia fedha hizo za TASAF.

Naye Joyna Sanga mnufaika ambaye ni mkazi wa Mbeya amesema mpango hupo sasa unawawezesha kusomesha watoto tofauti na ilivyokuwa awali.